Bilionea Mamelodi njia nyeupe Urais Caf

Muktasari:

Uchaguzi Mkuu wa Caf umepangwa kufanyika Machi 12 ukiwa ni moja ya ajenda za Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo ambao utafanyika Rabat, Morocco

Njia imeanza kuwa nyeupe kwa Mmiliki wa Mamelodi Sundowns, Patrice Motsepe kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) baada janausiku ya wagombea wawili wa nafasi hiyo Jacques Anouma na Augustin Senghor kutangaza kujiengua katika kinyang'anyiro hicho.

Senghor ambaye ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Senegal na Anouma kutoka Ivory Coast aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) walitangazwa kujitoa katika kile kinachodaiwa kumuunga mkono Motsepe.

Mpango wa Senghor na Anouma kujitoa unadaiwa kusukwa huko Morocco, wiki iliyopita ukiratibiwa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino ambaye anadaiwa anamuunga mkono waziwazi Motsepe katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Rabat, Morocco, Machi 12 mwaka huu.

"baada ya mapitio kadhaa na ushauri, nimeamua kujiondoa katika ugombea wa uchaguzi wa nafasi ya Urais ya Caf," alisema Anouma wakati alipotangaza uamuzi wake kupitia kituo cha luninga cha taifa cha Ivory Coast.

Kwa upande wake, Senghor alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kwa maslahi mapana ya mchezo wa mpira wa miguu barani Afrika.

"Kujiondoa kwangu katika ugombea wa Urais wa Caf kwa faida ya mgombea mwingine hakuwezi kukubalika na wote kwa sababu mbalimbali. Ninalifahamu hilo lakini naamini ni uamuzi mzuri, uamuzi sahihi," alisema Senghor katika taarifa yake.

Kujiondoa kwa Anouma na Senghor kunafanya idadi ya wagombea wa nafasi ya Urais ya Caf kwa sasa kubakia wawili tu ambao ni Motsepe na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Mauritania, Ahmed Yahya.

Hata hivyo kwa mujibu wa tetesi, Ahmed Yahya naye anaweza kutangaza kujiondoa katika kinyang'anyiro hicho na kumuacha Motsepe pekee atakayelazimika kusubiri kura za ndio au hapana pekee katika uchaguzi huo wa Caf unaosubiriwa kwa hamu.

Taarifa zinadai kuwa kwa mujibu wa makubaliano ya siri yaliyofikiwa, Motsepe atakuwa Rais wa Caf na Makamu wake watakuwa ni Yahya na Senghor wakati huo, Anouma akiwa mshauri wa Motsepe

Motsepe ni Nani?

Motsepe alizaliwa Januari 28, 1962 huko Pretoria, Afrika Kusini. Ana mke na watoto watatu na makazi yake yako Johannesburg, Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Forbes, Motsepe ana utajiri wa Dola 3 bilioni (zaidi ya Sh 6.2 trilioni) unaomfanya ashike nafasi ya tisa katika orodha ya matajiri barani Afrika huku kidunia akiwa nafasi ya 1513.

Chanzo kikuu cha utajiri wake ni biashara ya madini na uwekezaji katika sekta nyingine alioufanya.

Katika soka, Motsepe anafahamika kwa umiliki wake wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo aliinunua mwaka 2003.

Ni msomi wa shahada ya sheria katika madini na biashara aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand lakini pia ana shahada ya sanaa aliyopata katika Chuo Kikuu cha Swaziland