Bifu la Yanga, TFF tatizo lipo hapa!

Thursday April 08 2021
TFF pc
By Imani Makongoro

SERIKALI imeweka wazi mgogoro kati klabu ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) unaoendelea baada ya klabu hiyo kupeleka malalamiko yao Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kuilalamikia TFF kutoitendea haki.


Uongozi wa juu wa Yanga ukiongozwa na Mwenyekiti, Dk Mshindo Msolla jana ulifanya kikao na Serikali na kueleza malalamiko yao dhidi ya TFF kabla ya Wizara ya michezo kuwaita TFF na kutaka kujua tatizo ni nini.


Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo amesema Yanga iliwasilisha  malalamiko ya kutotendewa haki na TFF sanjari na waamuzi.


"Malalamiko ya Yanga yalikuwa nengi, tulikaa nao kikao kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8 Mchana, kubwa walidai kutotendewa haki na Shirikisho na waamuzi.


"Uongozi wote wa Yanga ukiongozwa na Mwenyekiti wao, Kaimu Katibu Mkuu, Mwanasheria na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walikuja," amesema.


Singo amesema robo saa baada ya kikao cha Yanga, Serikali iliwaita viongozi wa juu wa TFF ambao waliitikia wito wakiongozwa na Katibu Mkuu, Wilfred Kidao na Mwanasheria wao.

Advertisement


"Kikao na TFF kilianza saa 8:15 mchana hadi saa 10: 30 jioni, tuliwaeleza malalamiko ya Yanga na kikubwa ambacho TFF walisema ni kwamba wanafanya kazi kwa kufuata taratibu na wana kamati zao ambazo zinafanya kazi kwa weledi, hivyo kama kuna makosa yanatokea huko," amesema Singo na kuongeza walichokibaini ni 
kutoaminiana kwa pande zote mbili.


"Tumewaagiza wakae kikao cha pamoja Jumatatu wamalize tofauti zao, kisha watupe mrejesho wa kilichojiri kwenye kikao chao," amesema Singo.


Amesema TFF na Yanga wana shutumiana kwa vitu ambavyo vinaongeleka  na havihitajiki kwenda kwao, tatizo walilonalo ni kutoaminiana.


"Tumewataka kikao chao cha Jumatatu kimalize sintofahamu hiyo, Serikali haitakuepo, watakifanya wenyewe nasi watatupa mrejesho."

Advertisement