Bibi Diana aanzisha timu kocha mwenyewe

Muktasari:

Ili kuwa na timu bora katika Taifa na yenye ushindani ni vizuri kuwekeza katika kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto.

Dar es Salaam. Soka halina mwenyewe ndiyo ukweli huo baada ya bibi Diana Moshi (61) kuanzisha timu yake Dizonga na kuwafundisha watoto kucheza soka katika eneo Mbagala Kizuiani, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti online, Bibi Diana maarufu Bibi Bomba amesema ameamua kuunda timu ya watoto wenye umri wa miaka kumi na tano kushuka chini inayoitwa Dizonga.

“Wachezaji wengi wa timu yake ni wanafunzi wa shule za msingi kutoka kata ya Mbagala Kuu hasa kutoka shule ya msingi Kizuiani na Mbagala,” alisema Moshi

Alisema lengo kubwa la kujitolea ni kukuza vipaji vya watoto na kuviendeleza, kujenga nidhamu za watoto na kuwafanya watoto wajihusishe na michezo na kujiepusha na vitendo visivyofaa.

“Mimi ninapenda michezo kwa sababu michezo hujenga afya na pia nimewahi kushiriki mashindano ya Bibi Bomba kwa hiyo mimi ni Mwanamichezo kindakindaki na ninauwezo wa kucheza mpira na kupiga danadana.”

Alisema wazazi wa mtaa wa Kizuiani wamekubali na wameruhusu watoto wao kushiriki katika michezo baada ya kutoka shuleni.

Aliongeza kuwa watoto hao hushiriki mazoezi ya mpira wa miguu kuanzia saa kumi na nusu mpaka saa kumi na mbili na nusu jioni.

Bibi Bomba alisema pamoja na kufundisha, watoto hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kukosekana kiwanja, jezi na mipira.

“Ninaiomba serikali na wadau mbalimbali wamichezo kujitolea vifaa mbalimbali ili kuendeleza na kukuza vipaji vya watoto hawa kwa ajili ya kukuza sekta ya michezo hasa mpira wa miguu Tanzania na kumuunga mkono waziri  wa habari utamaduni Sanaa na  michezo, Dkt Harrison Mwakyembe amekuwa akisisitiza ukuzaji wa vipaji vya watoto.”

Moshi aliongeza kuwa ili kuwa na timu bora katika Taifa na yenye ushindani ni vizuri kuwekeza katika kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto.

Mchezaji wa timu hiyo Hassan Salehe alisema wameamua kujiunga na timu hiyo kwa sababu hawana chakufanya mtaani baada ya kutoka shuleni.

“Muda wa jioni baada ya masomo tumeamua kujihusisha na mchezo wa mpira wa miguu ili tujijenga kiafya, kiakili na kukuza vipaji vyetu kwa ajili ya kulitumikia Taifa letu hapo mbeleni kimichezo,” alisema Salehe

Salehe aliongeza kuwa wanafurahi kufundishwa na Mwalimu Moshi amekua akijitolea kuwafundisha bure.

Mkazi wa mtaa wa Kizuiani, Enrik Daudi alisema wameridhika na wanafurahi kuona watoto wao wanashiriki katika michezo.

“Mimi kama mzazi nina mtoto wangu ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Dizonga inayofundishwa na Bibi Bomba, lakini wachezaji hao hawana uwanja wa kufanyia mazoezi kwa hiyo ninamuomba mwenyekiti wa mtaa wa Kizuiani kuwapatia kiwanja,” alisema Daudi

Mwenyekiti wa mtaa huo, Mashaka Suleiman amekiri kuwepo kwa uhaba wa viwanja kwa watoto katika mtaa huo.

“Ninamfahamu bibi huyo anaejitolea kuwafundisha watoto mpira katika mtaa huu, lakini pia kuna uwanja chini Darajani ambapo vijana huwa wanafanya mazoezi kwa hiyo ninashauri vijana wapeane zamu ya kutumia uwanja huo na watoto hao.”