Biashara yasema iko tayari kwa lolote, kuondoka Dar kesho

Muktasari:

  • Hiyo ilikuwa ni mechi ya marudiano kwa Biashara United ambayo mchezo wa awali nyumbani ilishinda mabao 2-0.

Baada ya kuwa mguu ndani mguu nje kuendelea kucheza mechi za kimataifa, timu ya Biashara United umesema iko tayari kwa uamuzi wowote kutoka CAF.

Biashara ambayo sasa imeelekeza nguvu kwenye mchezo wao wa Jumatano wa Ligi Kuu, dhidi ya Prisons itaondoka alfajiri ya kuamkia kesho kuelekea Mbeya.

Mwananchi Digital ambayo imetembelea kambi ya timu hiyo iliyopo Lamada, Dar es Salaam iliwashuhudia baadhi ya wachezaji wakiwa kwenye vikundi vikundi, wakionekana kukata tamaa na ushiriki wao kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Biashara ilipaswa kucheza jana na Al Ahly Tripol ya Libya lakini ikakwama kuondoka nchini kwa wakati hadi muda wa mechi hiyo ulipopita.

Rais wa TFF, Wallace Karia amesema bado CAF hawajajibu ombi la timu hiyo la mechi yao kusogezwa.

"Watakapojibu tutasema, lakini mpaka sasa hakuna jibu lolote kutoka CAF,"  amesema Karia mchana huu.

Mwenyekiti wa Biashara United, Seleman Mataso amesema hivi sasa wanaelekeza nguvu kwenye Ligi.

"Tutaondoka saa 8 alfajiri ya kuamkia kesho kuelekea Mbeya, kama CAF watatuondoa kwenye mashindano, baada ya mechi zetu za Mbeya tutarejea nyumbani Musoma," amesema.

Amesema wako tayari kwa jibu lolote kutoka CAF,  kwani jitihada zao za kushiriki mashindano ya kimataifa zimeonekana.

Habari kutoka kwenye kambi hiyo zinasema, Biashara ilianza kukwama kutokana na ukata.

"Tulipanga kwenda Libya na ndege ya abiria, pesa ya tiketi ilikuwa tukope kwa GSM na tayari alikubalia, lakini kutokana na sababu za kiusalama ndege ile haikwenda Libya," alisema mmoja wa viongozi.

Amesema ndege ya kukodi ilikuwa ni changamoto kutokana na ukata, hadi pale Serikali ilipoingilia kati kwa Waziri Mkuu kutoa tamko.

"ATCL ililidhia kwenda kwa klabu kulipa Sh200 Milioni, ambazo tungekopeshwa, lakini ndiyo hivyo ilikosa vibali vya kupita kwenye anga za Sudan na Sudan Kusini na kutua kwenye uwanja wa ndege katika mji wa Benghazi ambako mechi hiyo ilitarajiwa kuchezwa.