Biashara wawapania Walibya

WACHEZAJI wa Biashara United wamepania kufanya kweli watakapokabiliana na na Al Ahly Tripoli ya Libya leo jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Biashara inakutana na Al Ahly Tripoli inayoonekana haina matokeo mazuri ugenini lakini imekuwa ikifanya vizuri nyumbani.

Katika michezo 10 ya mwisho ya mashindano ya kimataifa iliyocheza ugenini, Al Ahly Tripoli haijapata ushindi hata mara moja, ikitoka sare mara nne na kupoteza sita huku ikifunga mabao manne na kuruhusu mabao 12.

Wakati katika mechi 10 za nyumbani timu hiyo iliibuka na ushindi mara mbili, sare sita huku ikipoteza michezo miwili, hivyo Biashara United inatakiwa kupata ushindi mnono leo ili kazi yao iwe rahisi katika mechi ya marudiano Oktoba 23 nchini Libya.

Kocha wa Biashara, Patrick Odhiambo katika mazoezi ya siku mbili mfululizo alikuwa na kazi moja tu ya kuwanoa wachezaji wake kufunga mabao ya aina zote hasa kutumia mipira ya krosi na mashuti makali nje ya 18.

Katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa utaotumika kwa mchezo huo, Odhiambo alionekana kuwajenga wachezaji wake kimbinu, kuanzia kuzuia kwa pamoja pindi wanapokuwa hawana mpira na kushambulia kwa haraka.

“Tunahitaji kuzuia kwa pamoja lakini kushambulia kwa ushirikiano. Nimewajenga wachezaji wangu kwa yoyote kufunga pindi akipata nafasi. Licha kazi hiyo hufanywa na washambuliaji lakini hata mabeki, viungo wanatakiwa kutumia kila nafasi tutakayopata ili timu ipate ushindi,” alisema Odhiambo.


Wasikie Wachezaji

Nahodha wa timu hiyo Abdulmajid Mangalo, alisema; “Licha ya kukosekana ila hilo sio tatizo kwani wachezaji wenzangu wameahidi kuipigania Tanzania na kuonyesha tuna uwezo wa kupambana na timu kubwa bila kuhofia chochote.” “Mchezo ni mgumu kutokana na timu tunayocheza nayo ila benchi letu la ufundi wanawatambua vyema wapinzani wetu, hivyo imebaki kazi kwetu kama wachezaji kuonyesha uwezo wetu.”

Golikipa wa timu hiyo James Ssetuba, alieleza; “Timu nyingi hazitufahamu kwa sababu ni mara ya kwanza kushiriki michuano mikubwa Afrika, hii inatupa sisi faida ya kuweza kuwashangaza na kujulikana zaidi.”

Naye mshambuliaji, Atupele Green alisema; “Licha ya kwamba ni wageni kwenye mashindano ya kimataifa lakini tumejipanga kushangaza kwani najua wengi hawana imani na sisi hivyo tunataka kuonyesha tunaweza.”

Biashara United imefika hatua hiyo baada ya kuitoa Dikhil FC ya Djibouti kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 wakati Al Ahly Tripoli wao waliifunga Al Wadi SC ya Sudan kwa jumla ya mabao 4-0.

Imeandikwa na OLIVER ALBERT, DAUDI ELIBAHATI, CHARLES ABEL NA CLEZENSIA TRYPHONE