Biashara wao muhimu pointi tatu tu

KOCHA mkuu wa Biashara United, Aman Josiah amesema anajua ugumu wa mechi yao ya leo dhidi ya Cosmopolitan Fc kwani ni miongoni mwa timu zinazocheza soka la kuvutia lakini atahakikisha anatoka na pointi tatu.

Cosmopolitan Fc inaikaribisha Biashara kuanzia saa 10:00 jioni  mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Aman amesema lengo lao ambalo kama timu walipokuja jijini Dar es Salaam, ni kuhakikisha wanapata pointi sita zote na tayari wameshaweka mfukoni pointi tatu walizopata katika mechi na Green Warriors.

Aman amesema jambo kubwa ambalo anajivunia ni kuona hali ya ushindi ambayo wachezaji wake wanayo inawasaidia kuendelea kupambana katika kila mchezo husika.

"Tumetoka kuchukua pointi tatu kwa timu ngumu (Green Warriors) na ni mchezo wetu mfululizo kupata ushindi, najua wapinzani wetu walitusoma na kujua namna tunavyocheza;

"Lakini sisi tunaandaa timu kulingana na mchezo ambao tunakutana nao hivyo mechi itakuwa ngumu lakini tuna matumaini ya kupata pointi tatu."

Biashara imeshinda mechi tano mfululizo kwenye Ligi ya Championship ikizifunga, 2-1 Mbeya Kwanza, Ruvu Shooting 3-0, 3-1 Mbeya Kwanza, 3-1 Transit Camp na 3-1 Green Warriors.

Biashara Utd kwa sasa inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 14 huku Cosmopolitani yenyewe ikiwa nafasi ya 11 na pointi 14.