Biashara United, Yanga milango migumu Kirumba dakika 45

Wachezaji wa Biashara United na Yanga SC wakichuana kuwania mpira katika mchezo unaondelea uwanja wa CCM Kirumba.
PICHA NA HONEST MWANITEGA.

DAKIKA 45 za kipindi cha kwanza katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza zimeshuhudia kukiwa hakuna mbabe kati ya Biashara United na Yanga baada ya timu hizo kwenda mapumziko zikitoshana nguvu kwa suluhu (0-0).

Licha ya Yanga kufanya mashambulizi mengi lakini umakini katika eneo la umaliziaji umekuwa mdogo na kushindwa kuipa timu uongozi timu hiyo.

Wenyeji Biashara waliuanza mchezo huo kwa kasi ikitawala kwa dakika za mwanzoni ikitafuta bao la mapema lakini ilianza kupoteza umakini na taratibu Yanga kuanza kuuchukua mchezo na kumiliki dimba ikiwabana Biashara kila kona.

Yanga ilirejea mchezoni na kuumiliki ikisukuma mashambulizi yasiyo na ukomo langoni mwa Biashara United huku kandanda safi ambalo limeonyeshwa na mastaa wake likiwakuna mashabiki ambao walikuwa wakiwashangilia muda wote.

Mnamo dakika ya sita Yanga ilitengeneza shambulizi kali kupitia upande wa kulia kwa Chico Ushindi lakini krosi yake kumtafuta Dickson Ambundo ikawa ndefu na kushindwa kuzaa matunda.

Yanga ilipiga hodi tena langoni mwa Biashara United katika dakika ya 10 Chico Ushindi akikosa nafasi ya wazi yeye na kipa lakini akafumua shuti lililomlenga Daniel Mgore baada ya kupokea pasi nzuri ya mpenyezo kutoka kwa Farid Mussa.

Vinara hao wa ligi hawakukata tamaa waliendelea kusukuma mashambulizi tena katika dakika ya 13 ambapo Dickson Ambundo amekosa nafasi ya wazi akishindwa kuuzamisha mpira nyavuni akipokea pasi nzuri kutoka kwa Fiston Mayele.

Yanga iliendelea kuukamata mchezo na kuongeza kasi ya mashambulizi lakini umakini wa safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Fiston Mayele, Dickson Ambundo na Chico Ushindi ilishindwa kumalizia nafasi hizo ikiwemo iliyotengenezwa dakika ya 23 na 38 ambazo Ambundo alishindwa kuzimalizia.

Biashara imejaribu kutengeneza mashambulizi kadhaa kuelekea langoni mwa Yanga lakini imeshindwa kufurukuta mbele ya ngome imara ya ulinzi ya Yanga chini ya Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Djuma Shaban ambao mara zote wamedhibiti jitihada za Biashara.

Mchezo huo uko mapumziko ambapo utaendelea kwa dakika nyingine 45 zijazo.