Benchikha ataka mabao Simba

Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha ameweka wazi timu hiyo ina shida katika eneo la ushambuliaji baada ya kutofunga mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba kwenye mechi tatu za Ligi ya Mabingwa imefunga bao moja na kuruhusu nyavu zake zitikiswe mara mbili.

Lakini timu hiyo tangu ilipofungwa na Yanga 5-1, imefunga mabao matatu na kuruhusu mabao saba  kwenye mechi tano ilizocheza za mashindano yote.

Akizungumza baada ya kuwasili kwenye uwanja wa Julius Nyerere Terminal 3 akitokea nchini Morocco kwenye mchezo na Wydad Casablanca uliochezwa Desemba 9, Benchikha alionyesha wazi kutofurahishwa na pafomansi ya washambuliaji wake katika ufungaji.

Benchikha alisema kuna shida kwenye eneo hilo kwani wamefunga bao moja tu tena la penalti na yeye anachotaka kuona ni wakifunga zaidi.

"Kuna shida kwenye eneo la ushambuliaji, tumefunga bao moja tu la penalti, hatujafunga dhidi ya Jwaneng (Galaxy) wala Wydad na mimi nataka nione mabao yakifungwa;

"Tuna kazi ya kufanya kuhakikisha tunarekebisha makosa na tunapata mabao,  ninajiamini na wachezaji wangu waliopo kwenye kikosi changu hapa."

Benchikha alisema licha ya kutofunga anamwaga sifa kwenye eneo la kiungo kwani wamefanya kazi nzuri kwenye mechi mbili ambazo amesimamia za Ligi ya Mabingwa.

"Nina furaha na eneo hilo walikuwa vizuri wakimiliki mpira, kupiga pasi na hata kwenye kuchukua mipira upande wa upinzani walikuwa wanafanikiwa,"alisema kocha huyo.

Kocha huyo alisema licha ya matokeo waliyonayo hesabu kubwa anaziweka kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Wydad kuhakikisha anapata pointi tatu.

"Mchezo wetu na Wydad ni fainali kwetu, tunahitaji pointi tatu ili kufikisha pointi tano kwahiyo hakuna kingine kinachohitajika zaidi ya ushindi;

"Mashabiki wetu waje uwanjani kwa wingi kwenye mchezo huu kwa sababu ni fainali kwetu ili tuweze kusonga katika hatua inayofuata."

Benchikha kwenye mechi mbili zote ambazo amezisimamia, kocha huyo hajawa na mabadiliko kwenye kikosi chake.

Simba imecheza mechi tatu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Simba 1-1 Asec Mimosas, Jwaneng Galaxy 0-0 Simba na Wydad 1-0 Simba.

Timu hiyo ipo kundi B ikiwa na pointi mbili huku kinara ASEC Mimosas ikiwa na pointi saba.

Simba kabla ya kurudiana na Wydad AC itakuwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Desemba 15 kwenye uwanja wa Mkapa saa 10:00 jioni kisha itashuka uwanjani na Wydad AC kwenye uwanja huo huo Desemba 19, saa 10:00.



MECHI TANO ZA MWISHO SIMBA MASHINDANO YOTE
Simba 1-5 Yanga
Simba 1-1 Namungo
Simba  1-1 ASEC
Jwaneng Galaxy 0-0 Simba
Wydad AC 1-0 Simba