Beki yampasua kichwa kocha Uhamiaji
Muktasari:
- Uhamiaji ni timu ya nne kufunga mabao mengi Ligi Kuu Zanzibar sawa na Mlandege zilizomaliza na 46, huku KVZ ikiwa kinara ikifunga 60, ikifuatiwa na JKU (55) na KMKM (49).
WAKATI timu ya Uhamiaji ikiwa miongoni mwa zilizofunga mabao mengi Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2025-2026, kocha wa timu hiyo, Abdul Saleh amesema safu yake ya beki haikuwa bora kwa kuhimili mikiki ya wapinzani.
Uhamiaji ni timu ya nne kufunga mabao mengi Ligi Kuu Zanzibar sawa na Mlandege zilizomaliza na 46, huku KVZ ikiwa kinara ikifunga 60, ikifuatiwa na JKU (55) na KMKM (49).
Kocha huyo amesema Uhamiaji imekuwa timu yenye uwezo wa kushindana na kufunga mabao, lakini eneo la beki linahitaji kupewa kipaumbele zaidi msimu ujao.
“Baadhi ya mechi tulikosa matokeo mazuri baada ya safu ya beki kushindwa kudhibiti mashambulizi ya wapinzani, makosa madogo ya ulinzi yaliweza kuigharimu timu,” amesema.
Baada ya kutokea hayo, amesema Uhamiaji inapaswa kuweka mkakati wa kusajili mabeki wenye uzoefu, kujenga ushirikiano mzuri kati ya mabeki na kipa, pamoja na kufanya mazoezi maalumu ya ulinzi.
Mbali na hilo, kocha huyo amesema baada ya wachezaji wake tegemeo kuondoka kwenye kikosi hicho kwenda kwenye mafunzo, mambo yalibadilika na kujikuta timu kuyumba ikimaliza ligi nafasi ya tano, ikiruhusu mabao 27, huku ikifunga 46.