Beki Simba, Masai waongezwa Stars

Muktasari:
Taifa Stars inaendelea kujifua chini ya Kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije kwaajili ya mchezo wa marudiano na Kenya Jumapili.
BEKI wa kulia anayetajwa kujiandaa kurejea Msimbazi akitokea Lipuli ya Iringa, Haruna Shamte pamoja na wachezaji wengine wawili akiwamo Oscar Masai wameongezwa katika timu ya taifa, Taifa Stars kwa mechi ya marudioni dhidi ya Kenya, Harambee Stars.
Stars inatarajia kushuka dimbani Jumapili kurudiana na Kenya kwenye mchezo wa marudiano kufuzu fainali za Chan 2020 baada ya kutoka suluhu nyumbani wikiendi iliyopita.
Mbali na Shamte aliyekuwa kwenye harakati za mwisho kutua Msimbazi baada ya KMC waliomchomoa Lipuli ksuhindwa kumalizana na mabosi wa klabu yake ya Iringa, ameingizwa Stars kuchukua nafasi ya David Mwantika aliye majeruhi, pia walioongezwa ni beki wa kati wa Azam FC, Oscar Masai na kipa wa Polisi Tanzania, Mohammed Yusuph.
Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alisema ameamua kuongeza wachezaji hao baada ya baadhi ya nyota wake kukumbwa na matatizo na kushindwa kucheza katika mchezo wa kwanza.
"Kipa huyo kutoka Polisi anakuja kuziba pengo la Aishi Manula ambaye anasumbuliwa na nyonga na mkono na wengine ni kwa ajili ya Mwantika na Ibrahim Ajibu tayari nimewajumuisha kambini na tunatarajia kusafiri nao," alisema.