Beki Simba aibukia Kahawa Veterani ya Zanzibar

MABINGWA watetezi michuano ya soka ya Nyerere Day, Morogoro Veterani Fc imekubali kipigo cha kuchapwa bao 1-0 na Kahawa Veterani Fc ya Zanzibar katika mchezo mkali wa kusaka timu mbili za kutinga robo fainali, mchezo uliofanyika uwanja wa Shujaa mkoani Morogoro.

Licha ya Kahawa Veterani Fc kuibuka na ushindi huo dhidi ya wapinzani wao, mchezo huo umeibua vita kwa mlinzi wa zamani wa wekundu wa Msimbazi Simba Sc, Victor Costa Nampoka dhidi ya mshambuliaji wa zamani, Mokili Rambo aliyekuwa akikipiga Polisi Moro sasa Polisi Tanzani kwa wachezaji hao kukutana tena baada ya miaka 11 kustaafu soka la ushindani.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya kumalizika kwa mchezo mjini hapa,  Costa amesema mchezo huo dhidi ya wapinzani wao umemkumbusha namna alikuwa makini katika kumdhibiti, Mokili Rambo ili asipeleke madhara langoni kwao kila wanapokutana katika michezo ya ligi kuu Tanzania bara.

Costa amesema Mokili Rambo ni mshambuliaji hatari na msumbufu kwa walinzi na katika mchezo wa leo amehakikisha anatimiza majukumu ya ulinzi kwa mshambuliaji huyo ili asipeleke kilio katika chama lake la Kahawa Veterani.

“Mokili ni mshikaji wangu na jamaa yangu sana ni mshambuliaji nzuri, msumbufu kwa walinzi wa timu pinzani na anayejua kufunga na ukimwachia nafasi tu safu ya ulinzi lazima itanuna lakini leo mimi na wenzangu tumeweza kudhibiti safu yao ya ushambuliaji ya Morogoro Veterani wasilete madhara langoni kwetu.” amesema Costa

Costa amesema katika kipindi walichokuwa wakicheza ligi ya ushindani Simba Sc ilikuwa ikipata ushinda mara nyingi na mara chache maafande hao wakiambulia sare na michuano hiyo ya Nyerere Dar imemkumbusha kwa kukutana na wachezaji wenzake wa zamani ambao walikuwa wakikipiga katika vilabu mbalimbali.

Kahawa Veterani Fc imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kupata ushindi michezo miwili na sare moja ikikusanya alama saba na kuongoza kundi A lenye timu tano huku Morogoro Veterani Fc ikishinda michezo miwili na kipigo kimoja.

Bao pekee katika mchezo huo lilifungwa na mshambuliaji wa zamani ya Mtibwa Sugar, Abdallah Juma aliyekwamisha mpira wavuni kwa kichwa baada ya kazi nzuri ya, Hamis Kitwana.

Michuano ya Nyerere Day 2022 inashirikisha timu 18 za  mchezo wa soka, netiboli na michezo ya jadi kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Dodoma, Iringa, Zanzibar na Morogoro wenyeweji ikitimua vumbi katika viwanja vinne vya Morogoro Sekondari, Sabasaba, SUA na Shujaa.