Beki mpya Yanga Sh260 milioni

Chadrack Boka

Muktasari:

  • Baada ya mazungumzo FC Lupopo iliweka wazi mkwanja inaoutaka kwa ajili ya kumuachia beki huyo wa kushoto ambaye amekuwa tishio hasa kutengeneza nafasi na mipira ya krosi.

DILI la beki wa FC Lupopo ya DR Congo, Chadrack Boka limefikia patamu ambapo mabosi wake wanatarajiwa kutua Dar es Salaam wakati wowote ili kumalizia majadiliano ya mkataba na viongozi wa Yanga ili asajiliwe haraka.

Lakini, Mwanaspoti inajua kwamba katika dili hilo FC Lupopo imeitaka Yanga iweke mezani Dola 100,000 (takriban Sh260 milioni) ili kununua mkataba wake ambao umebakiza mwaka mmoja kumalizika.

Awali kupitia Mwanaspoti iliandika mchakato wa bosi kubwa wa Yanga ambaye alikuwa na mazungumzo na mabosi wa FC Lupopo nchini DR Congo ili kufikia muafaka wa kumpata staa huyo anayetajwa kuja kuchukua nafasi ya Joyce Lomalisa ambaye Yanga itaachana naye mwishoni mwa msimu huu.

Baada ya mazungumzo hayo FC Lupopo iliweka wazi mkwanja inaoutaka kwa ajili ya kumuachia beki huyo wa kushoto ambaye amekuwa tishio hasa kutengeneza nafasi na mipira ya krosi.

Taarifa za ndani kutoka katika kikosi cha FC Lupopo zinasema  mabosi wa timu hiyo watawasili dar es Salaam muda wowote kuanzia sasa ili ufanya makubaliano ya mwisho na uongozi wa Yanga.

"Yanga tumewapa ofa yetu kuhusu kununua mkataba wa mchezaji wetu nao wametupa mualiko wa watu wetu kuja Tanzania kuongea nao kwaajili ya makubaliano ya mwisho na watakuja wiki hii," kilisema chanzo kutoka timu hiyo ya DR Congo.

"Naona atakuja katibu mkuu wetu kuongea na Yanga wakikubaliana papo hapo watamalizana na kufanya huo uhamisho."

FC Lupopo imekuwa na uhusiano wa miaka mingi na Yanga na mwanzoni mwa miaka ya 2000 iliwahi kuiuzia mastaa Patrick Katalay, Pitchou Kongo na Alou Kiwanuka ambao walitamba kwa miaka kadhaa Jangwani. 

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema mabosi wa klabu hiyo watakutana na uongozi wa mchezaji huyo ili kumalizana nao ingawa tayari walishakubaliana kila kitu wakati wakiwa Lubumbashi.

Yanga imepanga kufumua kikosi na kukiweka sawa, ndoto ikiwa ni kucheza nusu fainali au fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Tayari imeshafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara majuzi na kubeba ndoo ya tatu mfululizo ambayo wamepanga shangwe lake likaanzie jijini Dodoma.

Mechi mbili za mwisho dhidi ya Dodoma Jiji na ile Prisons zitachezwa Dodoma badala ya Dar es Salaam ili kupanga gwaride la aina yake kuanzia bungeni mjini humo.