Beki Azam aingia rada za Wasauzi

Muktasari:
- Taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti inazo, zinaeleza mmoja wa wawakilishi wa kikosi hicho cha Afrika Kusini anavutiwa na uwezo wa nyota huyo, japo anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa timu nyingine tofauti zinazohitaji pia saini yake.
BEKI wa kati wa matajiri wa Dar es Salaam, Azam FC Abdallah Kheri ‘Sebo’ ameingia anga za Wasauzi baada ya kuanza kuwindwa na klabu ya Polokwane City ya Afrika Kusini kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho chenye makao jijini Polokwane katika jimbo la Limpopo.
Taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti inazo, zinaeleza mmoja wa wawakilishi wa kikosi hicho cha Afrika Kusini anavutiwa na uwezo wa nyota huyo, japo anakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa timu nyingine tofauti zinazohitaji pia saini yake.
“Bado sio rasmi ingawa ni kweli kuna wawakilishi wa Polokwane wanaomuhitaji Sebo, japo kama ambavyo ninakwambia na wao wanasema tu nje, ila hawajaleta ofa mezani kwetu ya kuonyesha wanauhitaji na mchezaji kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alipotafutwa kwa suala hilo, alisema ni habari za mitandaoni, japo suala la kurudishwa tena kikosini itategemea na mahitaji ya benchi lao la ufundi.
“Kwa sasa anacheza Pamba Jiji kwa mkopo, lakini siwezi kusema baada ya mkataba wake huo kuisha tutamrudisha au laah! kwa sababu hayo ni mambo ya kiufundi na itategemea benchi la ufundi lina malengo gani kwake na kwa wengine,” alisema Popat.
Mbali na Polokwane City inayomhitaji, timu nyingine ni Pamba Jiji anayoitumikia kwa sasa kwa mkopo ambayo pia inahitaji kumsajili moja kwa moja kwa ajili ya msimu ujao, kutokana na kukosa nafasi ya kucheza Azam katika kikosi cha kwanza.
Mwanaspoti linatambua, uongozi wa Pamba unahitaji saini ya nyota huyo aliyebakisha mwaka mmoja Azam, japo mojawapo ya masharti ya awali waliyokubaliana ni kuhakikisha kwanza timu hiyo inasalia tena Ligi Kuu Bara.
Awali, uongozi wa Azam ulimtoa mchezaji huyo kwa mkopo kwenda Fountain Gate katika dirisha dogo la Januari mwaka huu, ingawa Sebo aligoma na kuamua kwenda Pamba Jiji, jambo linalowapa kiburi mabosi wa TP Lindanda kumshawishi kubakia naye.
‘Sebo’ aliyetamba pia na timu za JKU, Zimamoto na Ndanda ni miongoni mwa nyota watatu waliotolewa kwa mkopo na Azam, pamoja na kipa, Ali Ahamada aliyeenda KMC na mshambuliaji, Adam Adam aliyetua Tanzania Prisons.