Prime
Baresi amtetea straika mpya

Muktasari:
- Baresi aliliambia Mwanaspoti, nyota huyo alichelewa wakati wa kuanza maandalizi ya msimu ‘pre-season’, hivyo itamchukua muda kidogo kuingia kikosini moja kwa moja kutokana na ushindani uliokuwepo.
KOCHA Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ ametolea ufafanuzi kutoonekana kwa mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Kelvin George aliyesajiliwa dirisha lililofungwa mwezi uliopita kutoka Bumamuru ya Burundi.
Baresi aliliambia Mwanaspoti, nyota huyo alichelewa wakati wa kuanza maandalizi ya msimu ‘pre-season’, hivyo itamchukua muda kidogo kuingia kikosini moja kwa moja kutokana na ushindani uliokuwepo.
“Ni mchezaji mzuri, lakini anahitaji muda kwani ukiangalia wengi wao hapa ni wazawa na wanafahamiana, ni vigumu kwake kuzoeana kwa haraka ila tukumbuke pia huu ni mwanzo na michezo bado ni mingi,” alisema Baresi na kueleza kufurahishwa na mwenendo wa timu hiyo iliyouonyesha hadi sasa ikiwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma ila bado ana kazi kubwa ya kufanya wakati anapoanza kutoka viwanja vya ugenini.
“Michezo mitatu imetuonyesha mwanga na jinsi ambavyo wachezaji na mashabiki zetu walivyotopokea, sasa hili ni deni kubwa kwetu kwao kwa sababu tunapaswa kuendelea kuonyesha thamani hii tunapotoka nje ya mkoa wetu,” alisema Baresi aliyeiongoza timu hiyo kushinda mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar na Ihefu na suluhu mbele ya Geita Gold na kuongoza ligi kwa muda kabla ya Yanga kurudi kileleni.
Timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu pamoja na JKT Tanzania na Tabora United, itasafiri hadi Ruangwa, Lindi kuvaana na Namungo katika Uwanja wa Majaliwa Septemba 30.