Barbara aonja joto la Yanga

ACHANA na matokeo ya mchezo wa jana wa Kariakoo Derby katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2021, unaambiwa homa ya pambano hilo zilianza mapema baada ya makomandoo wanaodaiwa kuwa wa Yanga kudaiwa kumvamia na kumshambulia Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez.

Mashabiki hao walivamia mara baada ya mazoezi ya Simba kumalizika juzi usiku kwenye Uwanja wa Amaan, kisha kumfanyia fujo Barbara ikiwamo kumvua ushungi na kupiga kichwani wakati akiongoza dua maalum ya kushukuru kumalizika kwa mazoezi yao uwanjani hapo.

Barbara amethibitisha kufanyiwa fujo hizo na kuripoti tukio hilo polisi, huku Jeshi la Polisi visiwani humo likithibitisha pia kutokea kwa jambo hilo na kueleza kuwa linawashikilia baadhi ya watuhumiwa wa vurugu hizo.

Tukio lilianza hivi. Juzi Jumanne, Simba na Yanga zilifanya mazoezi yao ya mwisho kwa ajili ya fainali za Kombe la Mapinduzi iliyopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa Amaan, huku mabaunsa waliodaiwa kuwa wa Yanga wakijikuta wakiangukia mikononi mwa polisi.

Yanga yenyewe ilifanya mazoezi yake kwenye Uwanja wa Mao kuanzia saa 11 jioni, wakati Simba ikipiga tizi Amaan kuanzia saa 1 usiku, mazoezi yote yakishuhudiwa na Mwanaspoti ambalo limepiga kambi kisiwani hapa kukupasha habari.

Baada ya mazoezi ya Yanga kumalizika gazeti hili lilishuhudia mazoezi ya Simba yaliyoongozwa na Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola pamoja na viongozi wa klabu hiyo na wa kwanza kufika uwanjani akiwa ni Crescentius Magori kisha kufuatiwa na Mohammed Nassoro ‘Mkigoma’ na Idd Kajuna na wengineo.

Baadaye Barbara naye alijumuika nao, lakini kabla ya mazoezi ya Simba kumalizika kulikuwepo na taarifa kwamba Yanga nao wangekuja kufanya mazoezi uwanjani hapo na kweli walifika na kulazimisha Simba watoke wafanya wao.

Viongozi wa Simba, wakati huo walikuwa wakiomba dua ili kuhitimisha mazoezi hayo, hivyo makomandoo hao wanaodaiwa kuwa wa Yanga waliamua kuwavamia uwanjani na kuwafanyia fujo kabla ya kudhibitiwa na wenzao wa Simba kisha kuja kudakwa na polisi.

Baada ya vurugu hizo, Barbara pamoja na viongozi wengine walilazimika kwenda kufungua jalada la kesi kwenye kituo cha Ng’ambo na kupewa RB yenye namba NGB/RB/247/2021 huku watuhumiwa wakiswekwa ndani usiku huo huo. Kwa upande wake, Barbara aliliambia Mwanaspoti jana kwamba, alivamiwa na watu hao wakati akiomba dua na kumfanyia fujo ikiwamo kumvua kitambaa alichojifunga na kumpiga kichwani, jambo ambalo lilimuogopesha kwa kuamini soka sio uadui.

“Bahati mbaya tukio la fujo limekuja ikiwa ni miezi michache tangu kupigwa kwa wanachama wetu mjini Morogoro na wenzetu, tunaona hili si jambo la kiuanamichezo na halipaswi kunyamaziwa ndio maana tumeripoti polisi,” alisema Barbara.

Mwanaspoti ilifika kituoni hapo ambako tukio limeripotiwa likiwa ni shtaka la kushambulia mwili. Hata hivyo, askari waliokuwepo kituoni waligoma kuzungumzia tukio hilo kwa undani kwa madai wao sio wasemaji wa Polisi na kutakata atafutwe Kamanda wa Polisi.

Hata hivyo, Kamanda huyo wa Polisi Zanzibar, Awadhi Juma Haji ambaye ofisi zake zipo Mademe alipoulizwa mapema mchana alisema hakuwa na taarifa juu ya tukio hilo.

“Kwangu halijafika labda baadaye nifuatilie kwani, muda huu nina kikao na pengine limeshughulikiwa kama kesi nyingine za kawaida ila litafuatiliwa na kutolea ufafanuzi,” alisema Kamanda Haji.