Bangala: Maxi kiboko yao

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Bangala alisema kama kuna watu wanadhani wameona makali ya Maxi basi wanakosea kwani jamaa hajacheza hata nusu ya kiwango chake ambacho anakijua.

YANNICK Bangala ambaye amekiri yuko kwenye hatua za mwisho kuachana na Yanga, ameangalia usajili wa mastaa 7 wapya waliotambulishwa mpaka sasa akasema winga Maxi Nzengeli atawakalisha wengi kutokana na ubora wake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bangala alisema kama kuna watu wanadhani wameona makali ya Maxi basi wanakosea kwani jamaa hajacheza hata nusu ya kiwango chake ambacho anakijua.

Bangala amefichua kwamba mapema msimu mmoja uliopita aliwahi kuzungumza na aliyekuwa kocha wa Yanga Nasreddine Nabi wakati akitafuta winga na alimpendekeza Maxi lakini baadaye akaona akaona alisajiliwa Tuisila Kisinda Yanga ikifuata uzoefu wake.

Bangala alisema Maxi ni mchezaji aliyekamilika ambapo katika nafasi zote za mbele anamudu kuzicheza kuanzia winga zote na zile nafasi mbili za umaliziaji na kiungo mchezeshaji wa kati.

"Nimemuona na namjua vizuri ni mdogo wangu, nina historia kubwa na Maxi tangu akiwa mdogo, nakumbuka nikiwa AS Vita niliwahi kumwambia kocha Ibenge (Florent) awachukue Kisinda na Maxi lakini baadaye akamchukua Kisinda peke yake,"alisema Bangala ambaye msimu wake wa kwanza Yanga aliibuka mchezaji bora wa ligi.

"Nilipofika hapa pia kuna wakati niliwahi kukaa na kocha Nabi akaniambia anatafuta winga nikamwambia amchukue Maxi lakini aliona kama bado anahitaji uzoefu nikaona alikwenda kumchukua Kisinda nilimuelewa.

"Maxi hapa bado hajacheza kabisa bado sana watu watashangaa zaidi kitu namuombea ni kuwa sawa kiafya lakini pia makocha wampe nafasi atasumbua sana hii ligi ya hapa subirini azoeane na wenzake.

"Mnachotakiwa kujua kuanzia namba nane kwenda mbele hizo nafasi zote jamaa anaweza kuzicheza vizuri tena sio kwa kubahatisha ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa sana, kwangu mimi huu ndio usajili bora mpaka sasa kwa niliowaona.

Aidha Bangala aliongeza kuwa watu wa Yanga watafurahia ubora wa pasi za Maxi lakini pia ujuzi wake wa kutoa pasi za mabao na hata kufunga mabao.

"Mnaona juzi alitoa pasi ya bao hiyo ni moja anaweza sana kutoa pasi zinazofika lakini anajua kufunga na kutoa pasi nyingi za mabao." Usikose mahojiano maalum na Bangala kwenye Mwanaspoti Jumamosi hii.