Bangala atua usiku, kuliamsha asubuhi hii

Yanga imempokea beki wake Yannick Bangala ambaye atafanyiwa utambulisho leo haraka kabla ya kuanza kazi.
SOMA: Watatu wapya watua Yanga
Bangala ametua jijini Marrakech jana usiku akifika moja kwa moja kambi ya Yanga iliyowekwa katika hoteli ya Kenzi hapa Marrakech ambapo alionekana wakati wa chakula na wenzake.
Beki huyo alionekana kuwa mchangamfu akipokewa na wachezaji wenzake wa DR Congo huku kocha wa timu hiyo akimlaki kwa furaha akisema:"oooh Yannick karibu sana:"
SOMA ZAIDI: Yanga yataka kutesti na Simba Morocco
Bangala ambaye anatua Yanga akitokea FAR Rabbat ya hapa Morocco alitakiwa kuwasili mapema lakini alikutana na changamoto za kuzuiwa Uwanja wa Ndege wa Instabul nchini Uturuki akitokea kwao Congo.
Hata hivyo mabosi wa Yanga hapa walizuia beki huyo asipigwe picha mpaka hapo atakapofanyiwa utambulisho maalum mapema leo kabla ya kuanza kazi haraka na timu hiyo.
Bangala alishasaini mkataba wa miaka miwili na Yanga mapema kabla hata hajaungana na timu hiyo akibakiza hatua moja tu kufanyiwa utambulisho kama ambavyo wachezaji wenzake 10 waliosajiliwa kipindio hiki.
Kuwasili kwa Bangala raia wa DR Congo ambaye anacheza beki wa kati kunaifanya Yanga sasa kubakiza mchezaji mmoja pekee kufika kambini kwao ambaye ni kiungo Khalid Aucho ambaye atatua kesho jijini hapa.
Beki huyo sasa anakamilisha idadi ya wachezaji 6 wa kutoka taifa moja la DR Congo akiungana na mwenyeji wao kiungo Mukoko Tonombe,winga Jesus Moloko, beki Djuma Shaban,wasshambuliaji Fiston Mayele na Heritier Makambo.