Bahanuzi acha miguu yako ifanye kazi
Pichani ni Said Bahanuzi, Mshamuliaji wa Polisi Morogoro
Muktasari:
Mechi hiyo iliisha kwa Simba kupata ushindi wa mabao 2-0 na yeye Adam Sabu maarufu kama Gerd Muller akifananishwa na mpachika mabao wa zamani wa Ujerumani, akiwa ndiye aliyetupia mabao yote mawili.
Katika moja ya hadithi zake nyingi alizokuwa akitusimulia yeye na Mzee Kilambo aliwahi kutupa kisa cha mechi iliyopigwa miaka ya sabini kati ya timu yake ya Simba na TPC ya Moshi.
Mechi hiyo iliisha kwa Simba kupata ushindi wa mabao 2-0 na yeye Adam Sabu maarufu kama Gerd Muller akifananishwa na mpachika mabao wa zamani wa Ujerumani, akiwa ndiye aliyetupia mabao yote mawili.
Sabu alituambia wakati ule Simba ilikuwa imemsajili kijana mmoja ambaye alikulia Morogoro wakati Sabu anacheza mpira kijana huyo alikuwa ni katoto kadogo mno, sasa ndiyo roho ya Simba chochote atakachosema viongozi watakuwa wanamsikiliza.
Kijana huyo alikuwa anaitwa Aluu Ally, kwa wale waliopata bahati ya kumwona bila shaka watakubaliana nami kuwa Aluu Ally ni mmoja kati ya viungo bora kabisa waliopata kutokea katika nchi yetu.
Wakati mchezo ulipomalizika Sabu akitoka na furaha ya kufunga mabao yote mawili Aluu Ally alitoka analia, hakupenda kabisa matokeo yale na viongozi wa Simba walipomfuata kumnyamazisha na kumuuliza kulikoni alijibu Simba ni timu kubwa huwezi kuwa na wachezaji wa aina ya Adam Sabu, nimempa mipira 18 pasi za uhakika anafunga mabao mawili tu.
Aluu Ally alisema kwamba hafai kuwepo katika timu kubwa kama hii, Sabu alilia sana baada ya kusikia kauli hiyo ya kijana huyo aliyemwacha Morogoro akiwa kinda kabisa.
Hivyo ndivyo soka lilivyo
Haraka sana nikamkumbuka Said Bahanuzi aliyepelekwa kwa mkopo Polisi Moro, nimeshuhudia mechi zake karibu tatu alizocheza akiwa na Polisi Moro, moja ikiwa ni pale kwenye Uwanja wa Mkwakwani, alikosa mabao mengi mno, mechi nyingine ni ya juzi tu tuliyoiona kupitia Azam Tv dhidi ya Kagera Sugar pale Uwanja wa Kambarage Shinyanga ambapo timu yake ilifungwa bao 1-0 na yeye Bahanuzi akiwa amepoteza baadhi ya nafasi za wazi mno.
Niliwauliza viongozi wake baada ya mchezo kwisha wakaniambia leo bwana afadhali, Mtwara dhidi ya Ndanda alikosa karibu mabao 10 ya wazi, vijana kina Bantu Admin, Mgangai kazi yao wenyewe ni kumpelekea tu Bahanuzi ashindwe na timu haina mashabiki, akikosa wanarudi kati kukaba.
Ni lazima nikiri kuwa miongoni mwa watu walioshiriki kumpeleka Bahanuzi Yanga kwa njia moja au nyingine alikuwa ni mwandishi wa makala hii, na kweli aliingia na kufanya vizuri mno katika michuano ya Kombe la Kagame na kuibuka mfungaji bora, basi na soka lake akaliacha katika michuano hiyo.
Baada ya hapo kukawa na hadithi nyingi zinazomhusu yeye za nje ya uwanja, maskini Bahanuzi hakupata mtu wa Saikoloji, jiji akaliingia kwa pupa, soka likamshinda, pamoja na kuitwa timu ya taifa bado kocha aliona mchezaji huyo alikuwa anahitaji marekebisho makubwa ili awe mchezaji wa timu kubwa.
Wiki iliyopita nilishtushwa kusikia Said Bahanuzi amekuwa mchezaji bora wa mwezi, nawaheshimu wataalamu hao wanaochagua wachezaji bora wa mechi lakini sikuelewa wana vigezo gani muhimu kumpitisha mchezaji huyo, ambaye kwangu naona amewanyima nafasi nyingi mno Polisi za kuibuka na ushindi na zaidi ya hilo naamini hata kama angeulizwa Kocha Mohammed Richard Adolf asingemtaja Bahanuzi.
Bahanuzi soka lake sasa limehamia mdomoni, kila kukicha anaeleza habari za ushirikina tu na anasahau soka na mambo hayo ni kiini macho tu na ninavyomfahamu Said ni mtu wa ibada mno, ni vipi aweke imani kubwa mno katika mambo ya giza? Ndiyo maana Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu wanapiga soka nje ya nchi kwa juhudi za mazoezi tu.
Ni kawaida ya wachezaji wengi mno wanaofikia umri mkubwa kuanza kuzungumza sana na mpira unahamia mdomoni zaidi kuliko kwenye miguu.
Kwa Bahanuzi umri wake bado ni mdogo, hivyo ana kila sababu ya kusahau mambo ya timu kubwa kama Simba na Yanga zenye mashabiki wengi wenye uwezo mkubwa wa kusoma timu zao na hawakosekani katika viwanja, lakini mbaya zaidi hawana subira na mtu wa aina ya Bahanuzi anayepata nafasi 18 na kufunga bao moja, hapo ndipo nilipomkumbuka kocha wangu Sabu.
Bahanuzi acha kuzungumza sana, piga soka watu wataona lakini kwa kiwango chako cha sasa binafsi bado napata shaka maana soka linachezwa uwanjani siyo chumbani, wote tunaliona na tayari umetoa masharti Yanga ikitaka urudi ikuhakikishie nafasi ya kucheza.
Kwa maana hiyo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amiss Tambwe, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho mmoja wao atupwe nje upewe wewe nafasi, hapo ndipo ninapochoka kabisa.
Mwandishi wa makala hii anapatikana Email [email protected]