Bado nyie sasa

SIMBA ileee makundi Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuing’oa Red Arrows ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-2 na fasta mashabiki wakawaambia Yanga, bado tuwapasue nyie sasa Desemba 11.
Simba wametinga hatua hiyo kwa mara ya kwanza licha ya kulala 2-1 ugenini Lusaka jana, shukrani kwa ushindi mnono wa 3-0 walioupata katika mechi yao ya awali nyumbani Dar es Salaam wiki moja iliyopita.
Mabao ya Red Arrows yaliyowekwa kambani na Ricky Banda dakika 45, pamoja na Saddam Phiri dakika 48 wakati la Simba likifungwa na Hassan Dilunga katika dakika ya 67.
Katika mchezo huo wa jana Simba walionekana kucheza kwa nidhamu hashwa dakika 40 za mwanzo katika kujilinda na kufanya mashambulizi machache ya kushtukiza kupitia, Dilunga na Bernard Morrison.
Muda mwingi Simba walikuwa wanajilinda ila walipoteza umakini huo dakika moja kabla ya kwenda mapumziko mabeki wake kushindwa kumkaba mpaka mwisho Banda aliyepata nafasi ya kupiga shuti kali na kufunga bao la kuongoza.
Simba bado wanakazi ya kufunga kwenye eneo la ulinzi pamoja na kukaba mipira inayotokana na krosi kwani bao ambalo alifunga Phiri lilikuwa la kichwa baada ya kuunganisha krosi.
Bao hilo ni la pili lilitokana na krosi kwenye kipindi cha hivi karibuni baada ya pia Simba kufungwa dhidi ya Geita Gold na straika George Mpole ingawa mwamuzi alilikataa na walifungwa tena bao la aina hiyo dhidi ya Jwaneng Galaxy na bado wameshindwa kuyapatia tiba.
Kocha wa Simba, Pablo Franco baada ya kuona mashambulizi yamekuwa mengi langoni kwake licha ya kucheza kwa kujilinda zaidi na kambani yameshakaa mabao mawili alilazimika kufanya mabadiliko ya kumtoa mshambuliaji Morrison na kumuingiza beki Shomary Kapombe.
Mabadiliko haya yalikuwa na maana ya kwenda kumsaidia, Israel Mwenda kukaba na kukata krosi nyingi zilizokuwa zinapigwa upande huo wa kulia kwa Simba mara kwa mara.
Morrison wa jana hakuwa yule wa mechi iliyopita nyumbani ambayo alikuwa nyota wa mchezo akifunga mabao mawili na kupika jingine, mbali na kukosa penalti. Lakini jana alikuwa amepooa kabisa.
Morrison jana alipoteza pasi na mipira mara kwa mara na mabeki wa Red Arrows hawakupata wakati mgumu kumzuia na alisababisha upande wake kushambuliwa zaidi kwani hakuwa anashuka kumsaidia Mwenda kukaba.
Mabadiliko aliyofanyiwa ya kuingia Kapombe yalionekana kuwa na tija upande wa Simba kwani hawakuwa wanashambuliwa zaidi upande huo kama hapo awali na mpaka kufanikiwa kupata bao muhimu kupitia kwa Dilunga aliyemlazimisha beki afanye makosa na kumnyang’anya mpira kabla ya kupiga ndizi iliyoenda kukaa kwenye nyavu ndogo ya mbali.
Baada ya kupata bao hilo, Franco alionekana kuzidi kuimarisha safu yake ya ulinzi na kucheza kwa kujilinda zaidi kwani alimtoa Bwalya na kumuingiza beki wa kati Joash Onyango katika dakika 74.
Dakika 82, alifanya mabadiliko mengine mawili yaliyokuwa na lengo la kujilinda walitoka, Dilunga na Kagere nafasi zao walichukua Mzamiru na Bocco.
Wenyeji Red Arrows walikuwa wanafanya mashambulizi ya mara kwa mara ili kupata bao la tatu kusawazisha matokeo ya mchezo wa kwanza lakini Simba walikuwa wakicheza kwa kubadilika kulingana na wapinzani wao walivyo.
MAMILIONI SIMBA
Shirikisho la soka Afrika (CAF), kwenye mashindano hayo wameweka utaratibu kwa timu ambazo zitafuzu hatua ya makundi na mpaka ile ambayo itakwenda kuchukua ubingwa kuna kiasi cha pesa wanachowapa.
CAF huwa wanatoa pesa hizo kwa ajili ya kuzisaidia timu kufanya maandalizi ya kutosha, kusafiri, hoteli pamoja na mambo mengine ya msingi wanapocheza mechi ya michuano hiyo.
Simba wao baada ya kutinga hatua ya makundi maana yake watavuta zaidi ya Sh Sh631 milioni kutoka (CAF) kwa ajili ya maandalizi pamoja na mambo mengi ya msingi na kama wakisonga hatua inayofuata watachukua kiasi kikubwa zaidi.
Kikosi cha Simba:
Aishi Manula, Israel Mwenda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ Henock Inonga, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Sadio Kanoute, Meddie Kagere, Larry Bwalya na Bernard Morrison.