Badiliko moja Stars ikiivaa Kenya

Benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' limefanya badiliko moja katika kikosi chake ambacho kimeanza dhidi ya Kenya katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu wa mashindano ya Chalenji yanayofikia tamati hapa Uganda leo.
Badiliko hilo limefanyika katika nafasi ya kipa ambapo David Kisu ameanzishwa badala ya Aishi Manula ambaye ni majeruhi.
Katika nafasi nyingine, Stars imeanza na wachezaji walewale ambao walikuwemo katika kikosi kilichoanza dhidi ya Uganda katika mchezo wa hatua ya nusu fainali.
Kikosi cha leo kinaundwa na David Kisu, Juma Abdul, Gadiel Michael, Bakari Mwamnyeto, Kelvin Yondani, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Ditram Nchimbi, Eliuter Mpepo na Nickson Kibabage.
Kwa upande wa Kenya, kikosi kilichoanza kinaundwa na wachezaji Samuel Odhiambo, Joash Onyango, Antony Wambani, David Owino, Samuel Olwande, Lawrence Juma, Abdallah Hassan, Johnstone Omorwa, Moses Mudavadi, Kenneth Muguna na Oscar Wamalwa.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Omar Abdulkadir kutoka Somalia ambaye atasaidiwa na Suleiman Bashir ambaye naye anatoka Somalia na mwamuzi msaidizi namba mbili atakuwa ni Liban Abdurazak kutoka Djibout.
Mwamuzi Ali Sabilla wa Uganda atakuwa refa wa akiba katika mchezo huo utakaoanza saa 7.00 mchana