Babu wa Loliondo aibukia Yanga

Monday January 23 2017
babu

Babu alijipatia umaarufu baada ya kuibuka na dawa ya ajabu

UNAKIKUMBUKA Kikombe cha Babu wa Loliondo? Watu walikuwa wanatoroka vitandani wanakwenda kunywa dawa ya jero kwa  Ambilikile Mwasapile.

Tiba hiyo iliyokuwa na jina ‘Kikombe cha Babu wa Loliondo’ iliaminiwa na watu wengi sana kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Afrika kwa imani ya kupokea muujiza wa kuponesha maradhi yakiwamo yale sugu.

Tabibu huyo aliyejinyakulia mamilioni ya shilingi, amekiri kuwa yeye ni miongoni mwa mashabiki wazuri wa Soka la Tanzania na haoni jinsi Yanga inavyoweza kukosa ubingwa msimu huu licha ya kwamba Simba ndiyo inayoongoza ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti mjini hapa, Babu alisema anaikubali Simba kwavile inapambana na ndiyo inayoongoza ligi ila Yanga itachukua ubingwa msimu huu.

Licha ya kuikubali Simba, Babu amesema haoni kama timu hiyo iko imara kuweza kuchukua ubingwa safari hii, anaona zaidi upepo ukielekea Yanga.

“Mimi naipenda Simba tena inanifurahisha zaidi kwa sababu inaongoza ligi na inafanya vizuri, inakuwa ngumu wakati mwingine kutabiri kwavile kunakuwa na mchuano mkali sana mara nyingi.

Advertisement

“Anaweza mwaka huu akachukua mmoja mwaka mwingine akachukua mwingine kati yao, Sijawaona siku za karibu kwavile televisheni yangu imeleta shida kidogo.

“Mi nawapenda wote, wanaleta changamoto sana kwenye huu mpira. Lakini msimu huu Yanga achukue na mwenzie achukue mwaka kesho,”alisisitiza Babu huyo kabla ya kucheka kwa nguvu.

Mbali na hilo Babu Mwasapile amezitaka timu nyingine zinazoshiriki ligi kufanya vizuri ili kuondoa dhana ya ubingwa lazima uchukuliwe na Simba au Yanga.

“Zaidi ya yote napenda zaidi timu inayofanya vizuri, lakini timu zenyewe zinabaki kuwa Yanga na Simba pekee hivyo  timu nyingine ziige mfano wa Azam ambao wamekuja kwa nguvu.”

“Kwa bahati mbaya televisheni yangu imeharibika muda sasa hivyo nashindwa kuangalia taarifa za habari na ligi hiyo,”aliongeza Babu ambaye matamshi yake yanatoa ishara kwamba yeye ni shabiki wa Yanga.

Babu amekuwa kimya kwa muda sasa akiendelea na mambo yake ya ujasiriamali kijijini kwake Loliondo, ingawa kwasasa anaonekana kuwekeza zaidi huku akiishi maisha ya kawaida kabisa ambayo ni ngumu kuamini kwamba alivuna mamilioni ya shilingi kwa kikombe chake.

Simba inaongoza Ligi Kuu Bara kwa pointi 45 huku Yanga ikifuatia kwa 43 na Azam ya nne ina pointi 31.

Advertisement