Aziz Ki kashindikana

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Aziz Ki, aliye kinara ya orodha wa wafungaji wa Ligi Kuu akichuana na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam mwenye 16, rekodi zinaonyesha amefunga mabao matano kwa mguu wa kulia, mengine 12 ya mguu wa kushoto zikiwemo friikiki tatu na penalti tatu vilevile, lakini cha ajabu hana bao lolote la kichwa.

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, sio mtu wa mchezo, kwani rekodi zinaonyesha anafunga eneo lolote na mguu wowote bila kutarajia, kama data zinavyoonyesha katika mabao 17 aliyofunga katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Aziz Ki, aliye kinara ya orodha wa wafungaji wa Ligi Kuu akichuana na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam mwenye 16, rekodi zinaonyesha amefunga mabao matano kwa mguu wa kulia, mengine 12 ya mguu wa kushoto zikiwemo friikiki tatu na penalti tatu vilevile, lakini cha ajabu hana bao lolote la kichwa.

Mabao hayo 17 aliyofunga nyota huyo wa Yanga, imemfanya afikie rekodi ya vinara wa mabao wa msimu uliopita, Fiston Mayele aliyekuwa Yanga na Saido Ntibazonkiza wa Simba walioibuka Wafungaji Bora, huku akiwa bado ana mechi mbili mkononi za kumalizia msimu ambazo mashabiki wa soka wanamsikilizia na Fei.

Kama Aziz KI atazitumia mechi hizo mbili za mwisho ikiwamo ya kesho Jumamosi itakayotumika kuikabidhi Yanga ubingwa wa msimu huu na ile ya Tanzania Prisons huenda mambo yakawa matamu zaidi kwa mchezaji huyo japo Fei Toto naye akiwa na mechi mbili dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar ili kumalizia pia msimu.

Hata hivyo, pamoja na kufumania nyavu huko, rekodi zinaonyesha kuna timu nne zilizomgomea nyota huyo kugusa nyavu za timu hizo, ikiwamo Mashujaa, Kagera Sugar, Coastal Union na maafande wa Tanzania Prisons itakayocheza na Yanga katika mechi ya mwisho Jumanne ijato kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Aidha, licha ya Aziz Ki kufikisha mabao 17 na kuifikia rekodi ya msimu uliopita ya Mayele ndani ya klabu hiyo ambaye kwa sasa yupo Pyramids ya Misri, lakini bado ana kazi ya kuvunja rekodi za mastaa wa kigeni ambao walifunga idadi kubwa zaidi ya mabao klabu katika msimu mmoja.

Mbele yake ana kazi ya kuvunja rekodi ya Amissi Tambwe ya msimu wa 2015/16 alifunga mabao 21, pia ipo ya misimu miwili ya Meddie Kagere wa Simba aliyefunga mabao 23 kisha 22 akitwaa tuzo ya mfu8ngaji mara mbili mfululizo, kitu ambacho hakijawahi kutokea kwa miaka mingi katika ligi hiyo.

Kagere alichukua kiatu cha ufungaji bora misimu miwili ya kwanza ndani ya Simba, 2018/19 mabao 23 na 2019/20 mabao 22, Yanga imebakiza mechi mbili dhidi ya Tabora United Mei 25 na Prisons Mei 28, huenda katika hizo Aziz Ki akavunja rekodi  hizo.


Timu alizofunga na aina ya mabao

Agosti 23, 2023 -KMC dakika 59 (mguu wa kushoto).

Agosti 29, 2023- JKT TZ dakika 50, friikiki (mguu wa kulia)

Oktoba 7, 2023-Geita Gold dakika 48 (mguu wa kulia).

Oktoba 23, 2023 hat-trick -Azam FC dakika 9 (friikiki mguu wa kulia), dakika 69 na 72 (mguu wa kushoto)

Novemba 5, 2023-Simba dakika 73 (mguu wa kushoto)

Desemba 16, 2023- Mtibwa Sugar P-dakika 45, 64 (mguu wa kushoto)

Desemba 23, 2023- Tabora United dakika 21 (frikikii mguu wa kushoto)

Machi 8, 2024- Namungo FC dakika 63 (mguu wa kushoto)

Machi 11, 2024- Ihefu dakika 68 (mguu wa kushoto)

Machi 14, 2024- Geita Gold dakika 54 (mguu wa kulia)

Aprili 14, 2024- Singida FG dakika 66 nje ya 18 (mguu wa kushoto)

Aprili 20, 2024- Simba penalti dakika 20 (mguu wa kushoto)

Mei 22, 2024) -Dodoma penalti dakika45, dk 51 (mguu wa kushoto).


WASIKE WADAU

Nahodha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema;  "Aziz Ki ameonyesha chachu ya ushindani kama mchezaji wa kigeni, kutokana na uwezo wa kuisaidia timu, hivyo anastahili kuwania kiatu cha Mfungaji Bora, ingawa naamini bato lao na Feisal Salum 'Fei Toto' litaenda hadi dakika za mwisho."

Mchezaji mwingine wa zamani wa klabu hiyo, Jerrson Tegete alisema; "Yanga imesajili majembe, ukiachana na Aziz Ki wapo wengi wanaofanya vizuri, pia naheshimu uwezo anaouonyesha Fei Toto, huku kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Haruna Moshi 'Boban' alisema; "Nathamini kiwango anachokionyesha Fei Toto na kuonyesha bato dhidi ya  Aziz ki, hivyo baina yao yoyote atakayechukua kiatu atakuwa amestahili.