Aziz Ki anogesha dili lake Yanga

Mshambuliaji wa ASEC Mimosas, Stephan Aziz KI.

Mshambuliaji anayetajwa kusajiliwa  na Yanga, Stephan Aziz Ki amekoleza hatua ya kukaribia Yanga baada ya kumtakia heri mgombea wa nafasi ya urais ndani ya klabu hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Ki ameweka kipeperushi cha mgombea Urais katika uchaguzi wa Yanga injinia Hersi Said huku akiandika kwa ufupi 'Kila la kheri Bosi'.

Hersi ndiye mgombea pekee wa nafasi hiyo ya urais ndani ya Yanga katika uchaguzi utakaofanyika Julai 9, 2022.

Kutokana na ujumbe huo wa KI naye Hersi amemjibu mshambuliaji huyo kupitia akaunti yake akiandika ahsante kijana wangu.

Hatua hiyo imezidi kuongeza uwezekano wa KI Kukaribia kutua Yanga ambayo inaelezwa wako katika hatua za mwisho kumleta raia huyo wa Burkina Faso.

Tayari KI ameshaagwa rasmi na klabu yake ASEC kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na mabingwa hao wa Ligi ya Ivory Coast.

Hersi ndio bosi wa Yanga aliyesafiri mpaka nchini Ivory Coast kufanya mazungumzo ya kumalizana na KI.

 Mapema  wawili hao walikutana nchini Morocco wakati ASEC ilipowafuata RS Berkane katika mchezo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwezi Aprili.