Aziz Ki akutwa na Covid Morocco

NYOTA wa Yanga na timu ya taifa ya Burkina Faso, Stephane Aziz Ki anatarajia kuripoti kambini Jumatatu ya wiki hii kutokana na changamoto za Covid-19 aliyoipata akiwa katika majukumu yake na timu ya taifa.

Aziz Ki alikuwepo kwenye kikosi hicho kilichocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Comoros uliopigwa Septemba 27, mwaka huu katika Uwanja wa Pere Jego jijini Casablanca nchini Morocco.

kwa taratibu za afya za Morocco wageni hupimwa Covid-19 kila baada ya siku tatu na Aziz Ki ni miongoni mwa wachezaji watatu wa Burkina Faso waliokutwa na maambukizi ya Corona baada ya kipimo hicho kufanyika baada ya mchezo.

Uongozi wa Yanga umefanya jitihada za kuwasiliana na chama cha soka cha Burkina Faso na kupata taarifa kuwa Aziz KI atafanyiwa vipimo vingine leo na kama mambo yakiwa mazuri atajiandaa na safari ya kurejea Tanzania kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan utakaopigwa Oktoba 8, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.