Azam v Yanga: Ni vita ya rekodi ya kibabe zaidi

Muktasari:
Tangu mwaka 2010 timu hizo zimekutana mara 18 na kila moja imeshinda mechi sita na zikitoka sare michezo sita, hivyo kuonekana hakuna mbabe wa mwenzake na hata katika mchezo wa leo timu yoyote ina nafasi ya kushinda.
AZAM itaikaribisha Yanga leo Jumamosi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaoanza saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya kibabe sana kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili ambazo zinawania ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Yanga inaikabili Azam leo ikitoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar kwa kukubali kipigo cha mabao 3-0 wakati wapinzani wao Azam walipata ushindi kwa kuifunga Lipuli mabao 2-0.
Kiwango kibovu ambacho ilikionyesha Yanga katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar kiliwapa wasiwasi mashabiki wao ambao waliohoji je wataweza kweli kupambana na Azam leo, lakini rekodi baina ya timu hizo mbili zinampa nafasi yoyote kupata ushindi.
Pia, mwenendo wa timu hizo kwenye Ligi Kuu Bara unaufanya mchezo baina yao kuwa mkali na wa kuvutia kwani katika mechi tano za ligi za hivi karibuni, Yanga imeshin mbili, imetoka sare michezo miwili na kupoteza mmoja wakati Azam katika michezo yake mitano ya karibuni, imeshinda mitatu, imetoa sare mchezo mmoja na kupoteza mmoja.
Vita ya ushambuliaji
Timu zote mbili zina washambuliaji hatari, Azam ikiongozwa an Shaban Iddi Chilunda, Donald Ngoma na Obrey Chirwa wakati Yanga itaongozwa na Patrick Sibomana, David Molinga, ambaye timu yake imesitisha maamuzi ya kumuacha kwenye usajili wa dirisha dogo.
Sibomana na Molinga ndio vinara wa mabao kwa upande wa Yanga wakiwa wamepachika wavuni mabao manne kila mmoja kama ilivyo kwa Chirwa wa Azam.
Kwenye viungo nako moto
Licha ya Yanga leo kumkosa Mohammed Issa ‘Banka’ anayetumikia adhabu ya kadi nyekudu lakini inajivunia safu bora ya kiungo itakayoongozwa na Haruna Niyonzima, Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama, Papy Kabamba Tshishimbi na Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambao, watakuwa na kazi kubwa dhidi ya viungo wa Azam watakaoongozwa na Salum Abubakary ‘Sure Boy, Frank Domayo na Brayson Raphael.
Yanga kwa siku za karibuni imekuwa ikibebwa sana na safu ya viungo ambayo imeonekana kucheza vizuri na hata kuipa matokeo timu hiyo hivyo, safu ya kiungo ya Azam inatakiwa kujipanga kama inataka kushinda mchezao huo.
Miaka 10 hakuna mbabe
Tangu 2010 hadi mwaka huu ni miaka 10 sasa imepita lakini timu hizo zimeendelea kuufanya mchezo baina yao kutotabirika kutokana na rekodi zao kwenye Ligi Kuu Bara.
Tangu mwaka 2010 timu hizo zimekutana mara 18 na kila moja imeshinda mechi sita na zikitoka sare michezo sita, hivyo kuonekana hakuna mbabe wa mwenzake na hata katika mchezo wa leo timu yoyote ina nafasi ya kushinda.
Msimu uliopita timu hizo zilipokezana ushindi, Azam ilianza kushinda kwenye mzunguko wa kwanza kwa kuichapa Yanga mabao 2-0 yaliyofungwa na Daniel Amoah na Mudathir Yahya kisha kwenye mzunguko wa pili, Yanga ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Mrisho Ngassa, ambaye ndiye ilikuwa mara yake ya kwanza kuifunga Azam tangu aanze kucheza soka la ushindani.
Azam mabeki, Yanga kiungo
Azam itawakosa mabeki wake mahiri wa kati Yakub Mohammed mwenye kadi tatu za njano na Aggrey Morris, ambaye hivi karibuni alifiwa na mkewe, hivyo kuna nafasi kubwa kwa Abdallah Kheri na Oscar Masai kuziba nafasi zao.
Kwa upande wa Yangaitamkosa Banka anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopata katika mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar, lakini kocha wa kikosi hicho Luc Eymael atapata ahueni leo kwa kurejea kikosini kwa beki wake wa kulia Juma Abdul, ambaye mchezo uliopita dhidi ya Kagera alikosekana kutokana na kuwa na kadi tatu za njano.
Kocha msadizi wa Azam, Iddi Cheche amesema wamejipanga vizuri kisaikolojia na kimazoezi kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo huo.
“Tunajua Yanga wametoka kupoteza mchezo uliopita, hivyo watakuja kwa hasira na nguvu dhidi yetu, lakini tumejipanga kuwakabili ili kuweza kupata ushindi.
“Naamini mechi itakuwa ngumu sana lakini malengo yetu ni kushinda na kupata pointi tatu muhimu katika mchezo huo.”
Matokeo
2010/2011
24/10/10 Azam 0-0 Yanga
30/3/11 Yanga 2-1 Azam
2011/2012
18/9/11 Azam 1-0 Yanga
10/3/12 Yanga 1-3 Azam
2012/2013
4/11/12 Azam 0-2 Yanga
23/2/13 Yanga 1-0 Azam
2013/2014
22/9/13 Azam 3-2 Yanga
19/3/14 Yanga 1-1 Azam
2014/2015
28/12/14 Yanga 2-2 Azam
6/5/15 Azam 2-1 Yanga
2015/2016
17/10/15 Yanga 1-1 Azam
5/3/16 Azam 2-2 Yanga
2016/2017
16/10/16 Azam 0-0 Yanga
1/11/17 Yanga 1-0 Azam
2017/2018
27/1/18 Azam 1-2 Yanga
28/5/18 Yanga 1-3 Azam
2018/2019
29/4/19 Azam 0-1 Yanga
28/5/19 Yanga 0-2 Azam