Azam na Simba vitani leo Kombe la Mapinduzi

Muktasari:
Azam na Simba walioapangwa kundi A pamoja na timu za URA ya Uganda, Mwenge na Jamhuri za Pemba, wataonyeshana ubabe kumtafuta mshindi anayefudhu kucheza hatua ya nusu fainali.
KIVUMBI cha Kombe la Mapinduzi huko Kisiwani Zanzibar leo Jumamosi kitakuwa kati ya Azam FC na Simba wanaocheza saa 02:15, usiku.
Azam na Simba walioapangwa kundi A pamoja na timu za URA ya Uganda, Mwenge na Jamhuri za Pemba, wataonyeshana ubabe kumtafuta mshindi anayefudhu kucheza hatua ya nusu fainali.
Matajiri hao wa lambalamba wanawania nafasi hiyo wakiwa na pointi sita baada ya kucheza michezo mitatu ambayo walishinda miwili na wakafungwa mmoja, wakati Simba wana pointi nne, wamecheza mechi mbili, wametoa sare mmoja na ushindi mmoja.
Ushindi unatakiwa kwa timu zote mbili ili kujiwekea mazingira mazuri kwani baada ya mchezo huo, Azam itakuwa imebakiza mechi mmoja na Simba mbili.
Mechi hiyo itachezwa baada ya ile ya kundi B ya saa 10:30 jioni, kati ya JKU ya Unguja na Singida mchezo ambao utakuwa ni wa kukamilisha ratiba kwa sababu Singida tayari ameshapita hatua ya nusu fainali pamoja na Yanga.