Azam, KMC ngoja tuone

AZAM FC ipo moto, KMC wapo vizuri na leo usiku zinakutana kwa mara ya kwanza msimu huu katika mechi ya Ligi Kuu Bara, huku mashabiki wakisubiri kuona nini kitakachotokea kwenye dakika 90 za pambano hilo.

Timu hizo zinakutana kuanzia saa 3 usiku, baada ya Bodi ya Ligi kuurudisha nyuma mchezo huo ambao awali ratiba ilionyesha ungepigwa kesho Ijumaa, huku kila moja ikiwa na kiu ya kusaka pointi tatu ili kuziweka pazuri kwenye msimamo.

Azam ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 22 baada ya mechi 10, ikifunga mabao 24 na kufungwa tisa, huku KMC ikishika nafasi ya tano ikiwa na pointi 19, ikifunga mabao 13 na kufungwa mabao 14.

Kama Azam itashinda mchezo huo itapaa hadi kileleni ikiing’oa Yanga yenye alama 24 kwa sasa, kwani Wana lambalamba hao watafikisha 25, lakini ikilazimishwa sare inaweza kuongeza pengo la pointi kati yao na Simba ilipo nafasi ya tatu na pointi 19 kama ilizonazo KMC.

Kwa namna timu hizo zilivyo na ushindani uliopo ni wazi haitakuwa mechi nyepesi, na kocha wa Azam, Bruno Ferry alisema mchezo huo ni muhimu kwao na anakutana na timu yenye msimu mzuri kwa sasa na anawaheshimu  kuhakikisha anapata matokeo mazuri.

Ferry alisema hata kama wakipata ushindi na kukaa kileleni bado wapinzani wao wana michezo michache hivyo ni wazi wanatakiwa kushinda kila mchezo ulio mbele yao.

“Wapinzani wetu wamekuwa na msimu mzuri sana hadi sasa kwahiyo najua kabisa tunaenda kukutana na ugumu.Tunataka kuhakikisha hatupotezi mipira kirahisi na ikitokea hivyo basi tuurejeshe haraka kwenye himaya yetu,” alisema Ferry aliyetoka kutwaa tuzo ya Kocha Bora wa Novemba, huku kocha wa KMC, Abdiamin Moalin alisema bado ana ukaribu wa hali ya juu na uongozi wa Azam lakini ana imani atachukua pointi tatu kwenye uwanja wao.

“Azam ni timu nzuri na imekuwa na matokeo bora kwa sasa na hata hawajapoteza mechi nyingi. Naamini wachezaji wangu ni wapambanaji na leo (jana) tumefanya mazoezi yetu ya mwisho na kikosi kipo vizuri,” alisema.

Rekodi zinaonyesha kwenye mechi 10 zilizopita baina ya timu hiyo, Azam imeshinda mara tano, huku KMC ikishinda tatu na michezo miwili ikiisha kwa sare kuonyesha mchezo wa leo ni vita ya kibabe baina yao.

Mbali na mechi hiyo, mapema saa 1:00 usiku, kutapigwa mchezo mwingine kwa wenyeji Namungo kuikaribisha Mtibwa Sugar inayoburuza mkia kwenye msimamo kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa, Lindi.