Aucho awagawa wadau tuzo za TFF

Muktasari:
- Ishu ya Aucho, imeonakana kuzua mjadala pamoja na muonekano wa baadhi ya tuzo kama vile ile ya mfungaji bora na hata kipa bora kutokuwa na utofauti wowote kama ilivyokuwa kwa mataifa yaliyoendelea huku ikilinganishwa na thamani ya ligi kwa sasa.
KITENDO cha jina la kiungo wa Yanga, Khalid Aucho kutokuwa kwenye orodha ya wachezaji walioteuliwa katika kikosi bora cha msimu uliopita wa 2023/24 kimewaibua wadau mbalimbali wa soka la Tanzania na kutoa maoni tofauti huku wengi wakiamini nyota huyo wa Uganda alistahili.
Pazia la Ligi Kuu Bara msimu uliopita lilifungwa rasmi jana, Alhamisi Agosti Mosi jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Super Dome Masaki ambako zilifanyika sherehe za tuzo za msimu huo.
Ishu ya Aucho, imeonakana kuzua mjadala pamoja na muonekano wa baadhi ya tuzo kama vile ile ya mfungaji bora na hata kipa bora kutokuwa na utofauti wowote kama ilivyokuwa kwa mataifa yaliyoendelea huku ikilinganishwa na thamani ya ligi kwa sasa.
Licha ya kuheshimu mchango wa Mudathir Yahya na uamuzi wa kamati ya tuzo, nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua anaamini, Aucho alistahili kuwa kwenye kikosi bora cha msimu.
Chambua amesema Mganda huyo ndiye namba sita wake bora msimu uliopita na ni wazi kuwa aliipa Yanga uhai katika eneo la kiungo tofauti na Mudathir ambaye alitumika zaidi katika kushambulia.
"Mudathir ni mchezaji mzuri sana lakini msimu uliopita hakutumika kama kiungo mkabaji, nadhani Aucho ndiye alistahili kuwa katika kikosi bora cha msimu kwa kigezo hicho kulingana na nafasi kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine ambao wamechaguliwa," amesema Chambua na kuongeza;
"Nadhani Mudathir alitakiwa kushindanishwa na wachezaji wa namba nyingine na hakupaswa kutazamwa kama namba sita lakini lazima tujue wanakamati nao ni binadamu na wana vigezo vyao katika machaguo yao, wamefanya kazi kubwa upungufu ni mchache."
Kwa upande wake, nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella hakutaka kuwa upande wowote zaidi aliheshimu uamuzi wa kamati kwa kusema wamefanya uchaguzi kwa vigezo vyao hivyo sio sawa kukosoa wakati hajui vigezo hivyo ni vipi.
"Nipo katikati naweza kusema Aucho alistahili au hakustahili, kwa sababu undani wa machaguo ya kikosi bora wanajua wanakamati," amesema kwa kifupi.
Kocha wa timu za vijana wa Azam, Mohammed Badru amesema mbali na Aucho alihoji pia tuzo ya kiungo bora, anaamini kuwa Feisal Salum alistahili na wala hakuna na shida juu ya uteuzi wa Stephane Aziz Ki kuwa mchezaji bora wa msimu (MVP).
"Kila mtu amekuwa akisema lake, kwanza tupongeze kamati kwa kazi kubwa waliyofanya, upungufu ni mchache sana naamini tuzo za msimu ujao zitakuwa bora zaidi, kwangu Aucho alitakiwa kuwa sehemu ya kikosi bora cha msimu na hata Fei nadhani ndiye kiungo bora," amesema.
Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema wachezaji wa Tanzania wanatakiwa kujituma wimbo anaouimba kila siku na ndio maana wageni wengi wanatwaa tuzo.
"Ubora na uwezo aliokuwa nao Ibrahim Ajibu hata Chama anasubiri sema kwa kuwa mwenzake anajua nini anafanya na ndio maana kila siku amekuwa akiongelewa," amesema.
WASHINDI WA TUZO HIZO 2023/24
Mchezaji Bora Ligi Kuu Bara - Stephane Aziz KI (Yanga)
Kiungo Bora Ligi Kuu Bara - Stephane Aziz KI (Yanga)
Mfungaji Bora Ligi Kuu Bara - Stephane Aziz KI (Yanga)
Beki Bora wa Ligi Kuu Bara - Ibrahim Bacca (Yanga)
Kipa Bora Ligi Kuu Bara - Ley Matampi (Coastal Union)
Mfungaji Bora Shirikisho - Clement Mzize (Yanga)
Mchezaji Bora Shirikisho - Feisal Salum (Azam FC)
Kipa Bora Shirikisho - Diarra Djigui (Yanga)
Mchezaji Chipukizi Bara - Raheem Shomary (KMC)
Mchezaji Chipukizi WPL - Ester Maseke
Kipa Bora WPL - Caroline Rufo
Mfungaji Bora WPL - Aisha Mnunka
Mchezaji Bora WPL - Aisha Mnunka
Kocha Bora Ligi Kuu - Miguel Gamondi
Kocha Bora WPL - Juma Mgunda
Mwamuzi Bora Bara - Ahmed Arajiga
Mwamuzi Bora WPL - Amina Kyando
Mwamuzi Msaidizi Bara - Mohammed Mkono
Mwamuzi Msaidizi WPL - Zawadi Yusuph
Tuzo za Rais TFF - Said El Maamry
Tuzo ya Heshima - Leodger Tenga
Tuzo ya Heshima WPL - Juma Bomba
Mchezaji Nje ya Nchi Wanaume - Mbwana Samatta
Mchezaji Nje ya Nchi Wanawake - Aisha Masaka
Mchezaji Bora Ufukweni - Jaruph Juma
Mchezaji Bora First League-Ayoub Masudi (African Sports)
Mchezaji Bora Championship - Edger William (KenGold)
Bao Bora la Msimu - Kipre Junior (Azam FC)
Kikosi Bora cha Msimu ni; Ley Matampi, Yao Kouassi, Mohamed Hussein, Ibrahim Abdullah, Dickson Job, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Feisal Salum, Wazir Junior, Stephane Aziz Ki na Kipre Junior.