ARSENAL NI AUBA

LONDON, ENGLAND. MUACHENI Mikel Arteta asherehekee. Asikwambie mtu, huduma ya Pierre-Emerick Aubameyang kwenye kikosi chake ni muhimu kwelikweli, hivyo kusaini dili jipya la kubaki Emirates tena kwa miaka mitatu ni habari ya kufurahisha kwa watu wote wa Arsenal.

Kwa msimu uliopita, Arsenal isingemaliza ndani ya 10 bora kwenye Ligi Kuu England kama wasingekuwa na huduma ya straika huyo wa Gabon kwenye kikosi chao. Bila ya Auba, Arteta angepata aibu kubwa. Kwa msimu huo wa 2019-20, Arsenal ilimaliza nafasi ya nane, wakikusanya pointi 56 - ambazo ziliwafanya kuwa jirani na Norwich City iliyokuwa nafasi ya 20 kuliko kuwakaribia mabingwa Liverpool.

Hata hivyo, kwa taarifa tu Arsenal ingekuwa kwenye vita ya kupambana kushuka daraja kama isingekuwa na huduma ya Aubameyang kwa msimu uliopita. Na sasa kuanzia mabosi hadi mashabiki wa timu hiyo ya Emirates wameshusha pumzi baada ya Aubameyang kusaini mkataba mpya utakaomfanya aendelee kuitumikia timu hiyo hadi mwaka 2023, huku akilipwa mshahara wa zaidi ya Pauni 350,000 kwa wiki.

Alifunga mabao 22 kwenye ligi msimu uliopita, akizidiwa bao moja tu na mshindi wa Kiatu cha Dhahabu, Jamie Vardy wa Leicester City. Bila ya mabao hayo ya Aubameyang, Arsenal ingekuwa na upungufu wa pointi 20 - hivyo ingekuwa na pointi 36 tu, ambazo zingewafanya wamalize pointi mbili tu juu ya timu zilizoshuka daraja - wangeshika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi, kwa mujibu wa compare.bet.

Katika awamu mbili tofauti msimu uliopita, Aubameyang alifunga mara mbili katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Everton na Watford. Bila ya huduma ya Auba kwenye mechi hizo mbili, Arsenal ingepoteza pointi sita. Aubameyang alifunga mabao ya ushindi kwenye mechi tatu tofauti, 1-0 dhidi ya Newcastle, kwenye 2-1 dhidi ya Burnley na 3-2 dhidi ya Aston Villa na hivyo kuichangia timu yake pointi za kutosha.

Mara nane nyingine tofauti kwa msimu uliopita, Auba alifunga mabao kusaidia Arsenal kupata sare, hivyo alichagia pointi nane timu yake kwenye mechi hizo kupitia mabao yake. Kwa ujumla wake, mabao yake yalichangia pointi 20 - na kama zisingekuwapo, basi Arsenal ingemaliza juu ya Aston Villa iliyonusurika kushuka daraja kwa tofauti ya pointi moja tu. Aston Villa ilimaliza na pointi 35, wakati Arsenal ingekusanya pointi 36 kama isingekuwa na huduma ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.

Bournemouth na Watford - ambazo zote zilishuka daraja ambapo zilishuka nafasi ya 18 na 19 mtawalia, zilipomaliza na pointi 34, mbili tu pungufu ya zile ambazo Arsenal ingevuna bila ya mabao ya Aubameyang. Hilo ndilo lililomfanya kocha Arteta kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha Auba anasaini dili jipya na kuendelea kukipiga kwenye kikosi chake.

Na sasa kwenye dili hilo jipya la miaka mitatu linamfanya Auba awe mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi huko Arsenal, Pauni 350,000 kwa wiki sawa na kiungo Mjerumani Mesut Ozil, lakini yeye atakuwa na bonasi nyingine kibao zitakazomfanya avune mkwanja mrefu zaidi.