Amir Maftah : Vigogo Simba, Yanga walinitibulia mambo
Muktasari:
Amir amefunguka mambo mengi ikiwemo jinsi vigogo wa Simba na Yanga walivyomtibulia mipango yake katika soka. Mbali na hayo nyota huyo ametaja matukio yaliyotokea kipindi anacheza kandanda, maisha yake kwa sasa na msimamo kwenye mpira kipindi hiki.
HUENDA jina la Amir Maftah limeanza kupotea vichwani mwa wadau na mashabiki wa soka nchini kutokana na nyota huyo wa zamani wa Yanga, Simba na Taifa Stars kutoweka muda mrefu kwenye kabumbu.
Beki huyo anakumbukwa kwa historia mbalimbali ikiwamo kuisaidia Taifa Stars kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), kwa mara ya kwanza mwaka 2009.
Amir anatoka katika familia ya mpira ikiwa na staa mkongwe Juma Amir Maftah aliyewahi kucheza Simba na Stars, Hussein Amir na Mrisho Michambo.
Beki huyo mwenye mwili mdogo kwa sasa yupo nyumbani kwao jijini hapa ambapo Mwanaspoti limefanya naye mahojiano na kueleza mambo kadhaa juu ya maisha ya soka.
Amir amefunguka mambo mengi ikiwemo jinsi vigogo wa Simba na Yanga walivyomtibulia mipango yake katika soka. Mbali na hayo nyota huyo ametaja matukio yaliyotokea kipindi anacheza kandanda, maisha yake kwa sasa na msimamo kwenye mpira kipindi hiki.
Mchezaji huyo ambaye alianza kucheza soka akiwa na umri mdogo na akiwa shule, alifanya maajabu mengi na alikuwa na uhakika wa namba kuanzia michezo ya Umitashumta na Umisseta.
Anasema nyakati hizo alishiriki michuano hiyo hadi ngazi ya Taifa, licha ya kwamba alikuwa na umbo dogo lakini aliupiga mwingi na kuwavutia wengi. “Umitashumta na Umisseta zote niliitwa hadi ngazi za Taifa na sikufanya mzaha, nilipiga mpira mwingi hadi shuleni kwetu ofisi ya mkuu shule ya sekondari (Moshi Tec) waliweka picha yangu,” anasema.
“Hizo picha zilikuwa ni za fainali ya Umisseta ambayo ilifanyika Mwanza na Rais mstaafu Benjamin Mkapa ndiye alifunga, na kutokana na udogo wangu na kipaji nilichokionyesha alishuka jukwaani kunipa mkono.”
Mkongwe huyo anaeleza kuwa kipindi hicho alikuwa na maisha mazuri kwani licha ya kucheza mpira darasani nako alitamba na kufikia kupewa mtu wa kumfanyia usafi.
“Nikiwa sekondari nilifurahia maisha kwa sababu nilikuwa na mtu wa kunifulia sare za shule, na nilipenda sana kusoma ili kufika mbali kama nyumbani walivyohitaji,” anasema.
Atengana na wazazi
Maftah anasema baada ya kuhitimu masomo ya kidato cha nne alihamia mkoani Arusha kwa shangazi yake, licha ya kwamba huko hawakuona thamani ya mpira.
Anasema kipindi akisubiri matokeo jijini Arusha, nyumbani kwao Mwanza wazazi walitaka aendelee na masomo wakitarajia baadaye awe mhandisi kutokana na masomo aliyosoma ya sayansi.
Anaeleza kuwa alikuwa haambiliki katika ishu ya mpira licha ya kwamba alikuwa na akili darasani na matokeo yake yalitoka akiwa amefaulu, ila soka alilipenda zaidi.
Amir anasema kutokana na kupenda sana mpira, wazazi walimshauri bila mafanikio, na waliamua kumtenga kwa mwaka mzima kwani walitaka we mhandisi. “Niliupenda sana mpira japo wazazi hawakutaka niache masomo kutokana na akili nilizokuwa nazo darasani na nilikuwa mtu wa sayansi, wakaamini nitakuwa mhandisi, nilipoonekana kuegemea soka wakanitenga mwaka mzima.”
Anasema katika pilika zake alikutana na mjomba wake ambaye alikuwa anafanya kazi Bodi ya Utalii, akamchukua kisha kuanza kufanya mawasiliano na wazazi wake ili kurejesha upya uhusiano.
Anasema mjomba wake alifanikisha uhusiano wao na kisha kumjumuisha kwenye kituo chake cha michezo cha Rolling Stone Football Foundation ambapo alikutana na wachezaji wengi.
Anasema alikaa katika kituo hicho akajifunza mambo mengi ikiwemo maadili ya michezo na kwamba, baba yake mzazi alikuwa hajui kama mwanaye anacheza mpira. “Mjomba wangu huyo alirejesha uhusiano baada ya kuzungumza na mama, nikakaa kituoni pale na kujifunza mambo mengi ya mpira, lakini Baba alikuwa hajui,” anasema Maftah.
Anasema mjomba alianzisha mashindano ambapo nyota huyo alikuwa katika moja ya timu iliyoitwa Arusha Meet FC, na walifika fainali na kubeba ubingwa wakafuzu michuano ya kanda na hapo baba ndipo alijua kuwa anacheza soka.
Anasema kwa muda huo soka lilimkolea na kuamua kuupa thamani na muda wa kutosha, na katika moja ya mashindano ya kanda mjomba wake alimkataza asicheze akidai sio saizi yake.
“Katika moja ya mashindano ya kanda nikiwa kituoni hapo mjomba alinikataza nisishiriki michuano hiyo ili aniandae kivingine nipate timu kubwa.
“Baba yangu alijua nacheza mpira kipindi cha mashindano ya mitaa ambapo tulibeba ubingwa na kufuzu michuano ya kanda ambapo mjomba aliona sistahili kushiriki ili anitafutie timu kubwa.”
Safari ya mpira yaiva
Anasema 2003, mjomba wake aliandaa mashindano ya vijana Afrika Mashariki na Kati, ambapo Amir alionyesha uwezo na kipaji kikubwa.
Amir anasema kupitia mashindano hayo aliitwa timu ya Taifa ya Vijana (U17), ambapo akiwa na nyota wengine walifanya vizuri kwenye michuano ya vijana na kufika fainali.
Mchezaji huyo anasema katika fainali ambayo ilifanyika Zanzibar walipoteza mbele ya Ethiopia na kushindwa kufikia malengo ya kubeba taji.
“Baada ya mashindano hayo timu nyingi zilinifuata zikihitaji huduma yangu licha ya kwamba nilikuwa mdogo na mjomba alikataa nisisaini popote kutokana na umri wangu.”
Anasema mwaka 2004 mjomba alimpeleka timu ya AFC pamoja na wachezaji wengine kutoka Rolling Stone ikiwa ni pamoja na David Mwantobe, Abdul Mtumwa, Salum Kibode na Omary Omary.
Anasema kipindi hicho AFC ilikuwa Ligi Kuu ambayo enzi hizo ilikuwa ikichezwa kwa makundi na kufuzu nane bora, ambapo waliiwezesha kufuzu.
Anasema katika msimu huo walikutana na Simba ambayo ilikuwa inashiriki Klabu Bingwa Afrika na kuifunga mabao 2-0, huku yeye akiibuka kuwa mchezaji bora wa mechi na kuzawadiwa viatu na pesa.
“Ulikuwa ni msimu wangu wa kwanza kucheza ligi hiyo na baada ya kufuzu, mchezo wa kwanza tulikutana na Simba kule Dar es Salaam na kushinda mabao 2-0 na kutangazwa mchezaji bora na kutuzwa viatu na fedha,” anasema.
Amir anasema baada ya msimu huo, timu nyingi zilimsaka ili kupata saini yake, lakini mjomba yake hakumruhusu kwenda popote na msimu uliofuata hakucheza popote ili kutafutiwa timu barani Ulaya.
Akwama Ulaya
Mkongwe huyo anasema wakati mjomba wake anafanya mawasiliano na baadhi ya watu huko Ulaya ili apelekwe kucheza soka la kulipwa, hali ilikuwa tofauti.
Anasema ikiwa ni dakika za mwisho dili lake likamilike, zilikuja taarifa za mmoja kati ya watu waliokuwa wakiwasiliana na mjomba wake kufariki dunia na mpango huo kufia hapo..
Amir anasema kuwa ishu hiyo ilionekana kumdhoofisha kiakili kwani awali aliamini anaenda kula maisha, huku mjomba wake akionekana kuumizwa zaidi na taarifa hiyo.
“Ilikuwa niende Ulaya kwa sababu mjomba alikuwa katika harakati za mwisho kunipeleka, lakini mmoja wa viongozi aliokuwa akiwasiliana nao akafariki dunia na safari ikaishia hapo,” anasema.
Anasema baada ya dili hilo kufa alikaa kwa muda bila timu akifanya mazoezi binafsi na baadaye akatoroka kusaini Mtibwa Sugar kimyakimya bila mtu kujua na hapo ilikuwa ni dirisha dogo la 2005/06. “Nilienda kusaini kimyakimya Mtibwa Sugar kipindi cha dirisha dogo na Mkurugenzi Jamal Bayser aliniambia nisaini muda mrefu kutokana na umri wangu mdogo, nilikubali badala ya miezi sita ikawa miaka miwili.”
Anasema alichobahatika ni kupata namba kikosini chini ya Kocha Mkuu Thom Olaba aliyesaidiana na Salum Mayanga, na alikutana na nyota mbalimbali.
Anasema kipindi hicho Nahodha alikuwa Mecky Maxime, lakini wengine wakiwa ni Zubery Katwila, Nizar Khalfan na Joseph Kaniki ambao wote walikuwa moto wa kuotea mbali.
Aitwa Stars
Anasema 2007 akiwa Mtibwa Sugar aliitwa Taifa Stars chini ya Maxio Maximo ambaye alimfuatilia kwenye mchezo baina yao na JKT Ruvu. “Nakumbuka ilikuwa mechi na JKT Ruvu ambapo Maximo alishuhudia mchezo huo akiwa jukwaani na tulishinda mabao 2-1 kule Dar es Salaam na lengo lake ilikuwa kusaka wachezaji wa timu ya Taifa,” anasema Bila yeye kujua chochote, Bayser alimpigia simu kuwa ameona jina lake, hivyo ajiandae kuitumikia nchi.
Anasema taarifa hizo alizipokea kwa furaha kwani hakuwa na fikra kuwa itatokea siku moja atavaa uzi wa timu ya Taifa na kwamba, hata wazazi wake walifurahi.
“Kipindi hicho tulienda kuweka kambi Brazil na kupata mechi za kirafiki kabla ya kuingia kwenye michuano ya Afcon ambayo hatukufanya vizuri mwaka huo.” Anasema 2008 aliitwa tena na Maximo ambapo Stars ilikuwa ikijiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ikiwa kundi moja na Msumbiji, Burkina Faso na Mauritius.
Anasema mwaka huo Msumbiji ndio walibeba ubingwa, huku Stars ikishika nafasi ya pili ambapo walicheza na Senegal kutoka kundi lingine na kuaga michuano baada ya wapinzani wao kuwatoa kwa jumla ya mabao 3-1.
Amir anasema pamoja na kutofuzu kilichovutia ni namna mashabiki walivyojaa uwanjani saa nne asubuhi kwenye dimba la CCM Kirumba. “Ndoto zetu zilipotea kufuzu hatua ya makundi kwa sababu nyumbani tulitoa suluhu, kule ugenini tukafungwa mabao 3-1,” anasema.
Stars yafuzu Chan 2009
Mkongwe huyo anasema baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo waligeukia ile ya Afrika wachezaji wa ndani (Chan) ambapo walifanya kweli.
Anasema katika mashindano hayo mchezo wa kwanza waliitungua Kenya mabao 2-0 nyumbani kisha ugenini wakatoshana nguvu ya bila kufungana.
Anasema raundi ya pili waliifunga Uganda mabao 2-1 nyumbani, huku ugenini wakishinda bao 1-0 na kufuzu kwa mara ya kwanza michuano hiyo.
kufukuzwa Yanga
Amir anasema baada ya kocha mkuu wa Yanga (wakati huo), Jacky Chamangwana kumhitaji kikosini na mfadhili wa timu, Yusuf Manji kumsajili, baadhi ya viongozi walimtibulia.
Anasema baada ya kutoka Mtibwa alijiunga na Yanga kwa kandarasi ya miaka mitatu, lakini alichokumbana nacho hawezi kusahau alichofanyiwa.
Mchezaji huyo anaeleza kuwa tangu alipojiunga na Yanga msimu wa 2008/11, wakati akielekea mwishoni kumalizia mkataba wake, mmoja wa vigogo Yanga alimfanyia kitu ambacho hawezi kusahau.
Anasema katika moja ya mechi zao dhidi ya Simba alicheza chini ya kiwango ambapo aliomba kufanyiwa mabadiliko, na hiyo Simba ilishinda 3-2.
Amir anasema kitendo cha kuomba kufanyiwa mabadiliko na matokeo ya mechi kumalizika kwa Yanga kupoteza, kigogo huyo alitangaza kuwa wapo baadhi ya wachezaji walihusika kuwahujumu.
Anasema hata mashabiki hawakuamini kilichotokea huku wakimtuhumu kuihujumu timu na kwamba, licha ya benchi la ufundi kuingilia kati kigogo huyo na mashabiki hawakuelewa.
“Yanga kupitia kwa (anamtaja jina) iliamua kunifukuza kwa madai niliwahujumu mchezo wa Yanga na Simba kwa kufungwa mabao 3-2, wakati niliona nacheza chini ya kiwango nikaomba kufanyiwa sub” anasema mkongwe huyo.
Anasema kitendo hicho kilimuumiza kwani taarifa zilisambaa nchi nzima ikidaiwa amehujumu timu na wakati akiwa Mwanza kwa mapumziko alipokea simu ya aliyekuwa dereva wa timu (Hafidh Salehe) akimtaarifu kuwa ana barua yake.
“Kipindi hicho Salehe alikuwa dereva akanipigia simu kuniambia ana barua kutoka kwa mwenyekiti, Iman Madega lakini siyo nzuri kwani ni ya kunifukuza, nikaona sina namna nikaondoka.”
Nyota huyo anasema alipokea changamoto hiyo licha ya kwamba Yanga ilimtangaza kimataifa, lakini ilimuathiri kisaikolojia kwa kitendo hicho.
“Kuna kipindi nilikutana na Madega nilimuuliza kuhusu ile barua ya kuihujumu Yanga hakuweza kunijibu, lakini naamini siku nikikutana naye tena nitamuuliza nione nini atajibu, kwa ujumla niliumia sana,” anasema.
Simba nao wamvuruga
Beki huyo kisiki anasema kuwa baada ya kufurushwa Yanga alijiunga na Simba katika dirisha dogo msimu wa 2010/11 ambapo mmoja wa vigogo, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ alimtaka kusaini kwanza miezi sita.
Anasema kutokana na uwezo wake alipofika Simba alifunga mabao mawili, huku akicheza kwa kiwango cha juu akiwa chini ya Kocha Patrick Phiri na kuwa kipenzi cha mashabiki.
Amir anasema kutokana na kile alichokifanya kwa muda mfupi, mabosi wa Msimbazi walimuomba kuongeza mkataba ili kuendelea kukipiga klabuni.
“Kwanza haikuwa rahisi mchezaji kufanya mabadiliko kwa timu za Simba na Yanga, kwa hiyo kwa kazi niliyoifanya hata Yanga wakaanza kunitamani nirudi, lakini nikawa nimeshaongeza mkataba Simba.”
Anasema hata Simba hakuweza kutoka salama kwani kati ya misimu mitatu, aliitumikia timu hiyo misimu miwili na ule wa mwisho ikamuwia vigumu kutokana na figisu alizofanyiwa.
mchezaji huyo anasema wakati mkataba umebaki mwaka mmoja, Azam FC walimpelekea ofa kutaka kumsajili, lakini Simba walimuwekea ngumu na hadi kufikia hatua ya kuondoka bila kulipwa Sh6 milioni za usajili wake. “Nilikuwa nimebakiza mwaka mmoja, Azam wakaja kutaka nijiunge nao, lakini Simba wakakataa nikajaribu kuomba pesa yangu viongozi wakaja na mipango ya kuipeleka timu Oman,” anasema.
“Kaburu ambaye alisimamia usajili wangu, akaniambia niungane na timu kwenda Oman kwenye kambi nikaweka msimamo kwamba wanilipe kwanza pesa yangu na hekaheka ikaanzia hapo.
“Timu ilienda Oman nikabaki Dar es Salaam na Kaburu akawa ananiambia niende ilipo timu na pesa yangu niikute huko nikakataa.”
Anasema baada ya timu kurudi Dar es Salaam, Amir hakupata namba tena akawa anakaa benchi na mwisho akaamua kuondoka huku akiacha pesa zake baada ya kufuatilia bila mafanikio.
Anasema 2014 baada ya kuona mambo yamekuwa magumu bila kuwa na timu, aliamua kutimkia Dubai katika Klabu ya Emirates na kushiriki michuano ya kampuni za mafuta ambayo hufanyika kila mwaka.
Anasema kwa sasa yuko huru na hana timu, huku akisisitiza kuwa bado hajazeeka na iwapo atapata timu wakaelewana yuko tayari kukipiga popote.