Ally Kamwe: Mabao 20? Simba sio dhaifu kihivyo

Muktasari:

  • Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salam leo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema mashabiki waondoe dhana ya kwenda kuifunga Simba mabao 20 kama wanavyofikiri kwa kuwa ni mechi ngumu.

KUELEKEA mechi ya watani wa jadi Machi 20, Yanga imesema haitaingia kwenye mchezo huo kwa kuwadharau wapinzani wao Simba kutokana na kupata matokeo mabaya kwenye mechi zao za karibuni.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salam leo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema mashabiki waondoe dhana ya kwenda kuifunga Simba mabao 20 kama wanavyofikiri kwa kuwa ni mechi ngumu.

"Ukienda kwenye Derby ya Kariakoo kwa mawazo kuwa umeshinda mechi tano mfululizo hii itakuwa ya sita utaingia chaka, ukienda Kwenye derby kwa mawazo kwamba mpinzani wangu ni dhaifu utaingia chaka," alisema Kamwe.

"Derby ina umuhimu wake, ina upekee wake na ina ugumu wake, sisi kama Yanga hatuitazami Simba kama ninyi mnavyoitazama, sisi tunaitazama Simba kama timu tishio ambayo tunawania nayo ubingwa, tunaitazama Simba kama timu yenye wachezaji wazoefu waliocheza michezo mingi mikubwa.

"Yanga tunaitazama Simba kama timu yenye viongozi makini, ukiniambia nitaje viongozi makini kwenye ligi, Simba siwezi kuwaacha, wanauzoefu na mipango ya kushinda mechi."

Kamwe aliongeza: "Hizo hadithi ambazo mnazo kwenye magrupu ya WhatsApp kwamba tunakwenda kumpiga mtu 20 nawaomba tuzibadilishe, naomba tuelekeze akili zetu kwenye kuchukua pointi tatu, hatutakuwa mabingwa kwa kumpiga Simba 100, tutakuwa mabingwa kwa kuwa na alama nyingi zaidi ya timu inayoshika nafasi ya pili."

"Novemba tano tulienda na mpango wa alama tatu bahati nzuri kwetu wakapiga mtu mkono, Jumamosi tunaenda kutafuta alama tatu ila wakijichanganya wakaamka vibaya tutalaumiana."

Katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, iliyopigwa Novemba 5, mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkapa, Yanga iliichapa Simba 5-1, mabao ya Kennedy Musonda, Max Nzengeli, aliyefunga mara mbili, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua kwa mkwaju wa penalti, wakati bao moja la kujifariji la Simba lilifungwa na Kibu Denis.