Aliyempiga ngumi kocha Mbeya City ataja sababu

Muktasari:

  • Ndizi alisema watu wengi waliona tukio lake ambalo lilikuwa la pili akiwa analipa kwa kocha huyo kumpiga mtama wakati anakwenda kushangilia bao lililofungwa.

Mbeya. Siku mbili baada Bodi ya Ligi (TPLB) kumfungia msimu mmoja kocha wa makipa wa Mashujaa, Shomary Ndizi na kutozwa faini ya Sh2 milioni kwa kosa la kumpiga ngumi Kocha wa Mbeya City, Abdalah Mubiru, ameanika kilichomsukuma kufanya kosa hilo.

Ndizi alisema watu wengi waliona tukio lake ambalo lilikuwa la pili akiwa analipa kwa kocha huyo kumpiga mtama wakati anakwenda kushangilia bao lililofungwa.

Alisema wakati anakimbia kwenda kuungana na wenzake alipofika eneo la benchi la ufundi la Mbeya City kocha huyo alimpiga mtama na kuanguka chini.

"Niliumia na kuchubuka lakini wakati narudi nami ndio nikafanya vile, hivyo wengi waliliona tukio la pili lakini lile la kwanza nililofanyiwa mimi hawakuliona.

"Napokea adhabu niliyopewa na bodi lakini nitakutana na uongozi wangu na kujadili zaidi juu ya hili lililofanyika kwangu kama ambavyo wengi wanalizungumza," alisema Ndizi.
 
Baada ya mchezo huo kumalizika aliyekuwa Mwenyekiti wa Mashujaa, Abdul Tika alisema wamesikitika kwa kitendo ambacho sio cha kiungwana kilichofanywa na kocha wao.

"Soka ni mchezo wa kiungwana sijajua kulitokea kitu gani hadi kufanya kitendo hicho ambacho sio kizuri na tayari hatua zaidi tutafuatilia ili kujua nini kipo nyuma yake," alisema Tika.

Kwa upande wake, Mubiru alisema hajawahi kuwa na ugomvi wa aina yeyote na kocha huyo sababu ndio kwanza walikutana kwenye mchezo na hakufurahishwa na tukio la kupigwa ngumi.

Alisema anashukuru hali yake inaendelea vyema baada ya matibabu hospitali akibainisha kuwa kiongozi huyo alimtafuta mara ya kwanza akamkwepa kabla ya kumrudia tena na kumpiga.

Hata hivyo Mashujaa imetozwa faini Sh500,000 katika mchezo huo kwa kukataa kutumia chumba cha kuvalia nguo huku Mbeya City ikimaliza msimu vibaya kila kona.

Mbeya City imetozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la watoto waokota mipira kuchelewa kwa makusudi kurejesha mipira kiwanjani kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliomalizika kwa sare ya 3-3 Uwanja wa Sokoine Juni 6.

Sambamba na hilo Mbeya City imetozwa faini Sh1 milioni kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa wachezaji wa Yanga wakati wakishangilia moja ya mabao waliyofunga katika mchezo huo.

Mbeya City imekumbana tena na rungu la faini ya Sh1 milioni kwa kosa la mashabiki wake kuwapiga na kuwasababishia majeraha shabiki wa KMC, Abdul Mohamed aliyekuwa amekaa jukwaani pamoja na afisa usalama wa timu hiyo, Seif Membe.

Katika mchezo huo uliochezwa Juni 13, kwenye Uwanja wa Sokoine na wenyeji kushinda mabao 2-1, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano kukwepa kushuka daraja.

Kutokana na tuklio hilo Mbeya City imeamuriwa kulipa faini ya Sh700,000 iliyotokana na Membe kupoteza simu yenye thamani ya Sh480,000 pamoja na fedha Sh220,000.

Ikumbukwe Desemba 2 Mbeya City ilitozwa faini ya Sh 500,000 kwa kosa la baadhi ya viongozi wake kumtolea lugha chafu mratibu msaidizi wa mchezo dhidi ya Simba ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Sokoine.