Al Ahly ndiyo ilivuruga ubingwa wa Yanga

Kocha Hans
Muktasari:
Akili zetu zishaganda kwa timu tatu za Simba,Yanga na Azam ingawa wengi wetu tuliwatoa Simba kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta ubingwa kutokana na aina ya usajili walioufanya na malengo waliyokuwa wamejiwekea.
WAKATI Ligi kuu ya Vodacom msimu wa mwaka 2013/2014 ilipokuwa inaanza mapema mwezi wa tisa mwaka jana kuna timu mbili tu ndizo zilikuwa zinaonekana kuwa zitafanya vizuri na kuchukua ushindi wa kwanza na wa pili, ilitokana na maandalizi pamoja na usajili mzuri waliokuwa wameufanya na kwa kutokuwa na hata wazo lolote juu ya timu gani mpya itakuja kufanya vizuri.
Akili zetu zishaganda kwa timu tatu za Simba,Yanga na Azam ingawa wengi wetu tuliwatoa Simba kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta ubingwa kutokana na aina ya usajili walioufanya na malengo waliyokuwa wamejiwekea.
Huku usajili kwa timu za Azam na Yanga ukionyesha jinsi timu hizo zilivyoanza kujizatiti kwa ajili ya msimu huo mpya bado timu ya Azam iliamua kuweka kambi ya maandalizi nchini Afrika Kusini na kufanikiwa kucheza michezo kadhaa ya kirafiki dhidi ya timu nzuri zinazocheza ligi kuu ya Afrika Kusini lakini uwepo wa wachezaji wengi waliokaa pamoja kwenye timu ya hiyo , matunzo mazuri wanayowapa wachezaji uliwafanya waanze vizuri na kumaliza ligi vizuri pia.
Kwa upande wa mabingwa watetezi Yanga ambao usajili wao ulilenga zaidi katika kuimarisha timu baada ya kumuongeza kipa mzoefu Deo Munishi ‘Dida’ ujio wa mchezaji wao kipenzi Mrisho Ngasa na usajili wa Hassan Dilunga uliwapa matumaini makubwa ya kufanya vizuri,Yanga ambao walianza kwa kishindo katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Ashanti waliyumba kidogo katikati ya ligi lakini wakafanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza wakiongoza ligi kuu,lakini mwisho wa msimu si Yanga waliofanikiwa kuvaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Ni vitu gani vilivyochangia kuwanyima taji hilo kwa mara ya pili mfululizo?
Falsafa ya Brandts
Kama ilivyo asili yake kocha huyo mholanzi nchi ambayo soka lake ni la pasi nyingi ingawa si soka la kasi kama zilivyo nchi nyingine,Yanga walikuwa na uwezo mkubwa wa kukaa na mpira kwa muda mrefu lakini hawakuwa na kasi walikuwa wanacheza taratibu na pasi ndefu.
Ndani yake kulikuwa na mfumo wa 4:3:3 ambao uliwategemea viungo watatu Athuman Idd, Frank Domayo na Haruna Niyonzima ambao walikuwa wakiwachezesha washambuliaji wenye mbio kama Mrisho Ngasa, Hamis Kiiza, Didier Kavumbagu au Simon Msuva na wachache kama Jerry Tegete,Nizar Khalfan , Husein Javu na wengineo.
Moja ya matatizo yaliyouvuruga mfumo huu ni kutokuwa na uwiano mzuri wa wachezaji wa kati ambapo mmoja kati ya viungo wa kati alikuwa mchezeshaji zaidi huku akisahau jukumu la ukabaji/kunyang’anya mipira.
Matokeo yake timu ikawa na viungo wanaokaba wawili,bado zaidi Haruna akawa ni mchezaji au kiungo anayechelewesha sana kuachia pasi kwa wafungaji wake,kosa hili la Haruna kukaa na mpira muda mrefu huku akicheza na jukwaa ilikuwa kasoro kubwa ambayo Brandts hakuwahi kumkosoa na hivyo kuacha wachezaji wengine wacheze kwa kufurahisha jukwaa badala ya kucheza kwa malengo.
Pia katika mfumo huu kulihitajika washambuliaji wawili wa pembeni wenye kasi ambao wanaunganishwa na mshambuliaji wa kati mwenye uwezo wa kukaa na mpira kitu hiki Yanga hawakuwa nacho washambuliaji wa kati kama alivyokuwa Kavumbagu au Tegete si wachezaji wanaoweza kukaa na mpira au wenye uwezo binafsi wa kujitegemea ambao wangeweza kulazimisha goli hata wakibaki na mabeki wawili.
Kosa jingine lililoigharimu Yanga ya Brandts ni ukweli kwamba kocha huyo aliwaacha wachezaji wajitawale wao zaidi na kujiona wapo hata juu ya kocha, nidhamu mbaya ya uchezaji kama timu yenye malengo kama mchezaji,kauli na ishara za kukataa maamuzi ya kocha kama walivyoonyesha Hamis Kiiza na Athumani Idd na zaidi upole aliokuwa nao kocha wakati mchezo ukiendelea vilichangia sana kuharibu nidhamu ya timu na wachezaji kwa ujumla.
La mwisho lilionekana chini ya kocha huyo ni wazi kuwa Brandts hakuwa mzuri katika kuusoma mchezo wa wapinzani na kujua tatizo la timu yake, hakuwa pia na wachezaji walioingia kutoka akiba wakiwa wazuri kwa maana ya kuingia na kuubadilisha mchezo ‘Super Subs’,hii ilijidhihirisha siku Simba waliposawazisha magoli yote matatu,lakini zaidi timu yake ilikuwa ikiendelea kupungua kasi ya uwanjani na hii ilitokana na Brandts kuiandaa timu kwa mazoezi ya mara moja kwa siku kitu ambacho kilipunguza nguvu ya uchezaji wa muda mrefu bila kuchoka.
Kuwatuhumu au kuwazomea wachezaji
Moja ya makosa ambayo wapenzi na washabiki wa timu ya Yanga hasa wale wanaokwenda uwanjani kuangalia michezo ya timu zao, ni ile ya kuwa wanaeneza habari za kuwatuhumu wachezaji wao pale inapotokea makosa ya kimpira ambayo yanatokea ndani ya mchezo,wachezaji kama binadamu wengine duniani nakokote hata huko kwenye ligi zilizo juu wanaweza kufanya makosa uwanjani si kunyang’anywa tu mipira bali hata kufungisha lakini bado wenzetu uwa wapole dhidi ya wachezaji wao,hapa Tanzania na hasa wapenzi wa Yanga wamekuwa na tabia ya kutokubali makosa yaliyofanyika uwanjani na wachezaji wao kuwa ni Bahati mbaya,badala yake huwafanya wachezaji wengi wanaojitolea kwa hali na mali kuifanya Yanga ishinde ambao kosa likitokea hukosa raha na kupoteza mapenzi ya kuichezea timu,wapenzi wa Yanga huwatuhumu wachezaji wao huku ligi ikiwa inaendelea wanasahau kuwa hao ndio wachezaji wao tegemeo ambao hata wafanye vipi lazima kocha wao atawapanga, walimpoteza kiakili na kwa muda Nadir Haroub,wakaja kwa Yondani wapo kwa Juma Kaseja,Tegete na wamemtuhumu sana Ali Mustafa,lakini hawa ni wachezaji wao si wachezaji wa Simba au Azam. Kibaya zaidi wamekuwa wakiwazomea na kumlaumu kocha kwa nini kampanga fulani,wameshamtoa mchezoni hasa katika dimba la Taifa Jerrison Tegete ambapo wapenzi/washabiki wa Yanga humzomea mchezaji wao akiwa anacheza,wanasahau kuwa hadi yeye kucheza katika kikosi kinachoanza ameshafanya mazoezi vizuri na kumshawishi kocha ampange mpenzi au mshabiki wa Yanga anapomzomea mchezaji aliye uwanjani haisaidii timu zaidi ya kuvuruga saikolojia ya timu,wapo wachezaji wa kiwango kikubwa duniani wanaokosa magoli zaidi ya Tegete hawazomewi! Yupo wapi Fernando Torres anayezomewa! Lakini wana Liverpool hawamzomei,hawa ndio washabiki waliopevuka wanaojua mpira ni nini?
Mechi za kimataifa
Yanga walishaamua kwa dhati kabisa kuwa mwaka huu walikuwa na lengo la kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa,walitangaza kabisa kuwa wamechoka kuwa wasindikizaji katika michezo hiyo na walikuwa na kila sababu ya kufanya vizuri kitaifa,usajili wa wachezaji wazoefu kwenye michezo ya kimataifa Emanuel Okwi na Juma Kaseja na ujio wa kocha mpya Hans Pluijm uliufanya uongozi wa Yanga pamoja na wapenzi wake kuamini kuwa wangefanya vizuri,ni wazi hasa baada matokeo mazuri ya mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya wacomoro na kutakiwa sasa kupambana na Al Ahly mawazo na akili za kila mtu wa Yanga zilihamishiwa katika mchezo huo,ziara ya Yanga katika kambi ya maandalizi nchini Uturuki nayo ililenga katika kuhakikisha kuwa Yanga inafika mbali kwa kuwatoa waliokuwa mabingwa wa Afrika,nguvu,akili na mbinu zilitumika kuiandaa timu yao na wakati Yanga ikiwekeza mawazo kwenye mchezo huo dhdi ya Al Ahly wenzao waliendelea kujipanga vizuri katika ligi ya ndani, kitendo cha Yanga kutolewa na Al Ahly bila shaka kilivunja morali ya wachezaji na hata viongozi,zile ahadi za pesa walizoahidiwa wachezaji wa Yanga zilitanda ndani ya vichwa vyao na hivyo ghafla timu ikawa nje ya mashindano,si rahisi kwa wachezaji kutulia mara moja hasa ukizingatia kwamba timu hiyo kubwa haina mtaalamu wa saikolojia, hiyo iliipelekea Yanga kutofanya vizuri katika michezo ya mwisho na huu ni ugonjwa unaoweza kuzipata timu hata kubwa ulaya.
Mfumo unaoweza kuzalisha magoli
Chini ya Hans Pluijm timu ya Yanga imefunga magoli mengi ambayo yalitokana na mfumo ambao kocha huyo alikuwa akiuutumia,kiuhalisia ni mfumo ulionyumbulishwa kutoka 4:3:3 na kuwa 4:2:1:3 ambao viungo halisi wanaokaba huwa wawili,mchezaji mmoja akicheza kama kiungo mchezeshaji nyuma ya washambuliaji watatu ambao kama wakitumika vizuri huzalisha magoli mengi,Yanga waliucheza vizuri siku walipocheza na Ruvu Shooting sababu kiungo nyuma ya washambuliaji alikuwa Mrisho Ngasa labda kwa uelewa mzuri alijua afanye nini,lakini siku zilivyozidi kwenda kocha alimchezesha Kiiza nyuma yao kazi ambayo hakuifanya, ni mfumo huo ambao huwafanya wachezaji wengi kupanda mbele na kwa mipira mirefu ya kushtukiza mara nyingi huwakuta wachezaji pengine watatu tu nyuma na hivyo kuwa rahisi kufungwa,aidha mfumo huu hushindwa kufanya vizuri pale timu pinzani inapoweza kujaza wachezaji wa kati zaidi ya wanne na hivyo kuwa rahisi kutawala sehemu ya kati.