Akpan nje wiki tatu

KIUNGO mkabaji wa Simba, Victor Akpan atakuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu na kumfanya akose maufundi ya kocha aliyemnoa akiwa Coastal Union, Juma Mgunda aliyejiunga na Wekundu hao wa Msimbazi kwa sasa.
Akpan alijiunga na Simba mapema msimu huu akitokea Coastal iliyokuwa chini ya Mgunda akiwa ndiye chaguo lake la kwanza kutokana na kumchezesha kikosi cha kwanza kwa msimu mzima ikiwamo kupiga shoo ya maana kwenye fainali ya ASFC dhidi ya Yanga iliyopigwa jijini Arusha, Julai 2.
Akizungumza na Mwanaspoti, Akpan alisema kuwa kwake nje ya timu kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mguu aliyoyapata katika michezo ya kirafiki iliyochezwa nchini Sudan kutamnyima fursa ya kuanza kazi upya na Mgunda ndani ya Simba.
"Nilicheza mechi moja tu dhidi ya Asante Kotoko kati ya michezo miwili ambayo Simba ilicheza Sudan ukiwamo wa wenyeji wa michuano hiyo maalum, Al Hilal na kuumia na jeraha hilo litaniweka nje ya uwanja kwa muda wa wiki tatu, japo naendelea na mazoezi mepesiĀ  gym," alisema Akpan na kuongeza;
"Najisikia vibaya kwa vile ninahitaji kucheza zaidi kutokana na kuingia kwenye timu hivi karibuni lakini ni mipoango ya Mungu nikiwa fiti nitarudi uwanjani kuendelea na majukumu yangu kama kawaida na nitafurahi kukutana tena na kocha Mgunda aliyeniamini tulupokuwa Coastal."
Akpan alisema anatamani angemkuta akiwa fiti ili aweze kumtumia kama alivyokuwa naye hapo awali lakini anaamini muda bado upo atakutana naye na kufanya kile anachokiamini kuwa anacho mguuni mwake.
"Nimepokea kwa furaha ujio wa Mgunda ndani ya Simba bahati mbaya amekuja kipindi ambacho nipo nje ya timu nikiuguza majeraha lakini naamini kwa muda ambao ntakuwa nje atakuwa bado anainoa Simba nitakutana naye," alisema na kuongeza;
"Ni kocha mzuri anauwezo mkubwa naamini ataisaidia Simba kufikia mafanikio kama amepewa muda mrefu wa kuinoa timu hiyo huku akisisitiza kuwa ni kocha ambaye anaamini katika vipaji na uwezo wa mchezaji."