AKILI ZA KIJIWENI: Simba wasilisahau kaburi la Magufuli Chato

Muktasari:
- Tunaweka akiba ya maneno maana Berkane sio timu nyepesi na ina uzoefu mkubwa na mashindano hayo maana imeshashiriki mara kibao na imewahi kutwaa ubingwa mara mbili huku ikiishia nafasi ya pili mara mbili.
MIMI na wenzangu hapa kijiweni hatujui na hatuna uhakika kama Simba itatetemesha Afrika kwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco ambayo itacheza nayo kwenye hatua hiyo.
Tunaweka akiba ya maneno maana Berkane sio timu nyepesi na ina uzoefu mkubwa na mashindano hayo maana imeshashiriki mara kibao na imewahi kutwaa ubingwa mara mbili huku ikiishia nafasi ya pili mara mbili.
Simba nao sio wanyonge japo hawajawahi kuchukua ubingwa lakini wana uzoefu mkubwa na mashindano ya kimataifa kwani kabla ya kufika hatua hiyo, wameishia hatua ya robo fainali mara tano tofauti kuanzia msimu wa 2018/2019.
Sasa kuna wazo fulani hapa likaibuika kijiweni kwamba kama Simba ikafanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano hayo basi ifanye ziara maalum ikiwa na kombe kwenda kuzulu kaburi la aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli.
Kwa kufanya hivyo itakuwa inaenzi sala nzuri ambayo marehemu Magufuli aliwaombea ya kutaka Simba iwe timu ya kwanza hapa Tanzaia kuleta ubingwa wa Afrika, ambayo aliitoa siku ile aliposhiriki sherehe za Simba kukabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika mchezo huo, Simba ilifungwa bao 1-0 na Kagera Sugar na hayati Magufuli aliwachana hadharani kuwa wanatakiwa wabadilike na wasicheze vile maana hawatoweza kufanya vizuri kimataifa.
Lakini mwishoni aliwaongelea kauli hiyo nzuri ya tumaini anataka wawe klabu ya kwanza hapa Tanzania kuleta ubingwa wa Afrika kwa vile wakijipanga hilo linawezekana.
Kama watafanikiwa kutwaa taji, Chato ambako Magufuli amelala usingizi wa milele sio mbali na wanamudu kabisa kufanya ziara ambayo itaonyesha wanathamini kile kilichokuwa kwenye ndoto zake na wamekipigania hadi kimetimia.
Hawezi kuamka kaburini akashangilia nao ubingwa lakini Simba itakuwa inaenzi na kuishi katika kile ambacho alikiamini na kukisema hadharani.