AKILI ZA KIJIWENI: Simba isijichanganye kwa Lomalisa

Muktasari:

  • Ninapokumbuka usemi huo, nikaanza kujisemesha peke yangu kuwa tetesi za Simba kutaka kumsajili beki wa kushoto wa Yanga, Joyce Lomalisa hazijaibuka kwa bahati mbaya hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika dirisha la usajili.

Wahenga walisema lisemwalo lipo na kama halipo li njiani laja.

Ninapokumbuka usemi huo, nikaanza kujisemesha peke yangu kuwa tetesi za Simba kutaka kumsajili beki wa kushoto wa Yanga, Joyce Lomalisa hazijaibuka kwa bahati mbaya hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika dirisha la usajili.

Inawezekana isiwe rasmi lakini usikute kuna watu fulani ndani ya Simba washaanza kuishawishi klabu hiyo imsajili Lomalisa ambaye hataongezwa mkataba mpya na Yanga baada ya huu wa sasa kumalizika.

Simuwekei kauzibe beki wa mpira Lomalisa lakini sioni sababu yoyote ya msingi kwa Simba kumsajili Lomalisa na nitawashangaa sana kama wataamua hivyo na hapo ndio nitaamini haina mpango wa kurudi katika makali yake.

Kuna haja gani ya kumsajili Lomalisa na kumlipa kiasi kikubwa cha fedha wakati huo tayari yupo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anayefanya vizuri kuliko hata huyo anayesajiliwa na takwimu na historia ziko wazi na zinathibitisha hilo?

Unapomsajili mchezaji wa kigeni unatumia kiasi kikubwa cha fedha kwa vile anatakiwa aje kutoa mchango mkubwa kikosini kwa maana ya matokeo na kuwapa darasa wale waliopo sasa ukiangalia Lomalisa hana ambacho amemzidi Tshabalala labda utofauti wa nchi tu ambazo wanatokea.

Hakuna haja ya kumsajili Lomalisa ambaye takwimu zinaonyesha amepiga pasi moja tu ya bao msimu huu huku akiachwa na wazawa kama Pascal Msindo, Rahim Shomary na Nickson Kibabage ambao pia wana umri mdogo kumzidi.

Itakuwa ni jambo la tija kwa Simba kuwasajili madogo wazawa ambao wameonyesha kiwango bora na takwimu zinawabeba kuliko huyo Lomalisa ambaye haonekani kama ataipa kitu kikubwa kulinganisha na aliyepo.

Halafu ukiangalia Simba inajenga timu ili kurudisha makali na mafanikio yake ambayo yamepotea hivyo inahitaji wachezaji ambao wataweza kulingana ubora na wale wa wapinzani wao Yanga na Azam sasa itakuwa jambo la ajabu kumsajili mchezaji wa kigeni ambaye ubora wake haujaweza kushawishi wapinzani wake kumbakiza na kumpa mkono wa kwaheri.