Aisee Mayele huku kadunda!

FISTON Mayele anatisha kutoka na kasi yake ya kufumania nyavu katika mechi za Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, lakini licha ya moto huo kuna mahali amekwama kabisa.

Mkali huyo mwenye mabao matatu ya Ligi Kuu na sita ya Ligi ya Mabingwa Afrika, licha ya kuzifunga timu 10 tofauti, lakini kuna wababe aliokwama kuzitungua ikiwamo Ruvu Shooting na Tanzania Prisons ameshindwa kabisa kuzigusa nyavu zao.

Msimu uliopita Mayele alifunga mabao 16 akishika nafasi ya pili nyuma ya George Mpole wa Geita Gold kabla ya msimu huu kuanza na moto, lakini timu hizo za maafande sambamba na Simba ameshindwa kabisa kuzigusa tangu msimu uliopita katika ligi.

Timu nyingine ambazo zina kazi ya kukomaa na Mayele ni Singida Big Stars na Ihefu zilizopanda Ligi Kuu msimu huu, kwani bado hajakutana nazo kama ilivyo kwa Prisons na Simba ambao hata msimu uliopita ilishindwa kuzifunga kama Ruvu na Polisi Tanzania ambazo safari hii zilifungwa na straika huyo kutoka DR Congo.

Rekodi zinaonyesha kwenye timu za msimu huu, Mayele ameshazifunga timu 10 ambazo ni Azam, Namungo, Kagera Sugar, Geita Gold, Mtibwa Sugar, Coastal Union, KMC, Dodoma Jiji, Polisi Tanzania na Mbeya City, huku zilizosalia zikiwa hazijamfanya ateteme uwanjani.

Simba licha ya kutofungwa kwenye ligi na Mayele, lakini imenyanyaswa mara mbili mfululizo kwenye Ngao ya Jamii kwa kufungwa msimu uliopita bao 1-0 na safari hii 2-1, yote akifunga yeye na kumfanya afikishe mabao matatu katika mechi hizo mbili.

Hapa chini ni mechi ambazo Mayele alikwama kutupia nyavuni katika Ligi Kuu, licha ya umahiri wake;


YANGA v RUVU

Hapa ndipo historia hii ilipoanzia mchezo huo ulichezwa Benjamin Mkapa Novemba 2, 2021 na Yanga kushinda mabao 3–1 yaliyowekwa kimiani na Feisal Salum, Djuma Shaban na Mukoko Tonombe.

Kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Lake Tanganyika, Kigoma siku ya Mei 4 mwaka huu, uliisha kwa suluhu. Msimu huu tena katika mechi iliyopigwa mwanzoni mwa wiki, Ruvu iligoma tena kumpa ujiko Mayele licha ya timu hiyo kupasuka mabao 2-1.

Katika mchezo huo, mabao ya Yanga yaliwekwa wavuni na Feisal Salum na Bakari Mwamnyeto na sasa kinachosubiriwa ni mechi ya marudiano itakayopigwa Februari 5 mwakani. Mayele atatetema au la!


YANGA v TZ PRISONS

Tanzania Prisons haikuruhusu bao mbele yake.

Mara ya kwanza ilikuwa Desemba 19, 2021 zilipokutana Nelson Mandela, mjini Sumbawanga Rukwa na Yanga licha ya kushinda 2-1, lakini Mayele alitoka kapa.

Mabao ya Yanga yaliwekwa kambani na Feisal Salum na Khalid Aucho na kwenye mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Mei 9 mwaka huu ngoma iliisha kwa suluhu na kumfanya Mayele atoke bila kutetema. Kwa msimu huu timu hizi hazijakutana, kwani mchezo wa kwanza baina yao utapigwa Desemba 4 na marudiano utapigwa mwakani.


YANGA v SIMBA

Mayele licha ya kuwa na zali la kuwalaza mapema mashabiki wa Simba kwa kufunga mechi mbili za Ngao ya Jamii ikiwamo ya msimu uliopita iliyokuwa derby yake ya kwanza, lakini jamaa akachemsha mbele ya Mnyama katika Ligi Kuu Bara.

Baada ya kufunga katika Ngao ya Jamii iliyozindua msimu uliopita, Mayela alishindwa kutetema kwenye michezo yote miwili ya msimu huo iliyoisha kwa suluhu ikianza ile ya Desemba 11, 2021 na ule wa marudiano uliopigwa Aprili 30, 2022.

Kwenye uzinduzi wa msimu huu, Mayele alitupia mabao mawili katika mechi ya Ngao ya Jamii na sasa anasubiriwa na mashabiki kuona atachemsha tena mbele ya Mnyama katika mechi ya Kariakoo Derby inayotarajiwa kupigwa Oktoba 23 mwaka huu palepale Kwa Mkapa.


WASIKIE HAWA

Mwanaspoti lilizungumza na baadhi ya makipa na mabeki waliokutana na mziki wa Mayele na kupambana naye kumzuia asiteteme mbele ya timu zao.

Beki Dotto Shaaban wa Prisons alisema; “Mbinu kubwa iliyotufanya tufanikiwe kumzuia Mayele kwa mechi mbili zilizopita ni kuzingatia maelekezo ya kocha, licha ya ukweli jamaa ana kiwango cha juu na anatisha ukikutana naye uwanjani, kwani ni mpambanaji.”

“Tunaenda kukutana na Yanga Desemba, kazi yetu itakuwa ni ile ile kumzuia asifunge na pia tusipoteze mbele yao, kama tulivyofanya mechi ya mwisho baina yetu iliyoisha kwa suluhu,” aliongeza Dotto, huku kipa Mohammed Makaka aliyekuwa Ruvu na sasa anakipiga Mtibwa Sugar, alikiri Mayele ni mshambuliaji hatari, ila anashukuru hajawahi kutunguliwa naye.

“Mayele kushindwa kutufunga kwa kipindi kile nafikiri ilikuwa ni bahati kwangu na umakini wangu niliouweka wakati analilenga lango kwa kupata zaidi ya nafasi mara moja, ila alishindwa kutumbukiza mpira wavuni, japo tulipoteza mechi ya kwanza na nyingine kuisha kwa suluhu.”

Beki wa Ruvu Shooting Frank Nchimbi amezungumzia namna alivyoweza kumdhibiti mshambuliaji huyo.

“Tuliambiwa kuwa makini na Mayele ila nashukuru kazi aliiona na nafikiri hatausahau mtiti wangu,” alitamba.

Mayele alikiri kuna timu hajazifunga na roho inamuuma, ila ana nafsi ya kusahihisha kama dhidi ya Polisi, lakini msimu huu aliwapasua mapema tu katika mechi ya ufunguzi wa msimu huu.