AFL yasema sheria ya bao la ugenini ipo palepale

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya African Football league kuelekea mchezo wa kesho kati ya Al Ahly dhidi ya Simba lile bao la ugenini lipo.

Kanuni ya 15 kifungu kidogo cha tatu kimeondoa sintofahamu hiyo ikiweka wazi kwamba kwa mechi za hatua ya robo fainali, nusu fainali timu itakayokuwa na idadi kubwa ya mabao ya ugenini itafuzu hatua inayofuata.

Kanuni hiyo hiyo kipengele kinachofuata ikaeleza kuwa bao hilo la ugenini linatumika mpaka kwenye mchezo wa fainali ambapo timu yenye mabao mengi baada ya mechi ya pili itachukua ubingwa.

Kwa upande wa kanuni ya 16 kipengele cha kwanza nacho kimeeleza kuwa kuanzia hatua ya robo fainali endapo timu zote zitalingana kwa mabao ya kufunga na yale ya ugenini mechi hiyo itaamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Ufafanuzi huo unaifanya Simba kesho kuendelea kuupigania ushindi kwenye mchezo huo wa ugenini au sare ya mabao 3-3 na zaidi ili iweze kutinga hatua ya nusu fainali.

Simba ililazimishwa sare ya mabao 2-2 hapa nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Ahly ambao ni mabingwa wa Afrika na kesho saa 11 jioni timu hizo zitamalizana kwa mchezo wa pili wamarudiano utakaopigwa Jijini Cairo nchini Misri.