AFCON 2023 itampaisha Fei Toto

KIUNGO wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ametabiriwa makubwa kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazoanza rasmi kesho Jumamosi huko Ivory Coast, ikidaiwa zitambeba nyota huyo aliyepo kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Stars inashiriki michuano hiyo kwa mara ya tatu baada ya zile mbili za 1980 na 2019, huku Fei zikiwa ni fainali za pili kwake baada ya kushiriki mara ya kwanza zilipofanyikia Misri.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Zanzibar, Kocha Mkuu wa JKU, timu iliyomuibua Fei kabla ya kutua Yanga, Salim Ali Haji, alisema : “Namuona Fei akifika mbali, hasa akizitumia vyema mechi za Afcon kuna timu zitaanza kumtafuta, kule mataifa mbalimbali yanakutana, hivyo kuna viongozi wengine wa timu wanakwenda kwa lengo la kuangalia wachezaji ambao baadaye watawasajili.”

“Fei ana kipaji sio kwamba katengenezwa ukubwani, umri pia unamruhusu, ni kujitambua zaidi na kuwa na ndoto za kucheza timu zaidi ya Azam na isiwe hapa Tanzania sasa, uzuri wa Azam hawana choyo pale atakapopata timu nje ya nchi.”

Kocha wa JKT Tanzania aliyewahi pia kumnoa akiwa JKU, Malale Hamsini alisema; “Angekuwa mchezaji mwingine angekuwa ametoka kwenye reli hadi sasa hivi kutokana na mambo aliyoyapitia, uzuri Fei anajitambua nini anataka katika kusoka kulinda kipaji chake.

“Alipambana kuhakikisha anaisaidia timu yake, anasaidia kulinda kipaji chake na kurudi timu ya Taifa na sasa anashiriki fainali za Afcon ambako kuna nafasi kubwa ya kupata ulaji kama atapewa nafasi ya kucheza na yeye akaonyesha uwezo mkubwa.

“Fei ana nidhamu kubwa na mpira, anapaswa kuendelea kuilinda nidhamu hiyo itamsaidia, Afcon wachezaji wanaocheza wametoka mataifa ambayo soka lao liko juu hivyo wachezaji wetu watakutana na mastaa wanajua wanataka nini, naamini ataweza kuuza kipaji chake kupitia hiyo,” alisema Malale

Kiungo huyo amesajiliwa Azam akitokea Yanga, usajili wake ulikuwa ni wa kuvutana kwa sababu timu yake hiyo ya zamani haikutaka kumwachia.

Zilianza kama tetesi za kutua Azam lakini baada ya mvutano huo akatua kwa matajiri hao wa Ligi Kuu rasmi msimu huu ambako sasa anafanya vizuri.

Awali, hakuwa na mwanzo mzuri ndani ya Azam kutokana na kukaa nje ya uwanja muda mrefu lakini sasa kiwango chake kimerudi na kinaonekana kuongezeka zaidi kutokana na namna anavyofanya kwani hadi sasa amefunga mabao nane na asisti nne.

Jisajili kwenye tovuti ya Mwanaspoti kusoma kila habari kiganjani mwako popote ulipo kwa gharama nafuu.