Adidas inavyohaha kutaka kumhamisha Messi Barca
Lionel Messi
Muktasari:
Kampuni hiyo imekuwa katika upinzani mkubwa na kampuni ya Nike ambayo kwa sasa inaidhamini Barcelona kitendo ambacho kimeifanya Nike iinase sura ya Messi kiulaini katika matangazo yake.
KWA mujibu wa habari za ndani kutoka kwa wakala maarufu wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Francois Gallardo, kampuni ya vifaa vya michezo, Adidas, imekuwa ikihaha bila ya mafanikio ikitaka kumhamisha staa wa Barcelona, Lionel Messi, kwenda Bayern Munich au Chelsea.
Kampuni hiyo imekuwa katika upinzani mkubwa na kampuni ya Nike ambayo kwa sasa inaidhamini Barcelona kitendo ambacho kimeifanya Nike iinase sura ya Messi kiulaini katika matangazo yake.
Tayari Messi ana mkataba binafsi na Adidas na amekuwa akitumia viatu vyake, lakini klabu yake ya Barcelona inadhaminiwa na Nike kitu ambacho kinamfanya avae jezi yenye nembo ya Nike.
Kutokana na hali hiyo, Adidas ilijaribu kuitumia Bayern Munich katika kumnasa Messi na inasemekana katika dirisha lililopita, wababe hao wa Ujerumani walitoa ofa ya Euro 250 kwa Barcelona.
Ofa hiyo ipo katika kipengele cha mkataba wa Messi Nou Camp na inamruhusu kuondoka klabuni hapo. Adidas ilikubali kuisaidia Bayern kulipa nusu ya pesa hizo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa staa huyo anatua Ujerumani na kuvaa jezi ya Bayern yenye logo ya Adidas.
Achilia mbali Bayern, Adidas ilikuwa tayari kufanya mpango huo kwa timu tatu huku Bayern ikiwa mojawapo.
“Adidas iliweka kiasi cha Euro 125 milioni, nusu ya pesa za mauzo ya Messi katika mkataba. Nusu nyingine ingelipwa na klabu yenyewe na klabu tatu zilikuwa tayari. Moja ilikuwa Bayern na labda watajaribu tena Juni mwakani,” alisema Gallardo.
“Wiki ijayo nitaitaja timu ya pili na siku nikiitaja timu ya tatu nadhani soka la Hispania litatingishika sana.”
Nguvu ya uhamisho wa Messi kwenda Bayern ilikuwa inatiwa chachu na uhusiano mzuri uliopo baina ya kocha mpya wa timu hiyo, Pep Guardiola na Messi. Kocha huyo ndiye aliyemwendeleza Messi na kuwa mmoja kati ya wanasoka bora kuwahi kutokea duniani.
Guardiola pia ana urafiki wa karibu na kampuni ya Adidas jambo ambalo mabosi wa kampuni hiyo waliamini lingesaidia katika kuhakikisha Messi anatua Allianza Arena.
Matokeo yake, Bayern ilitoa ofa ya Euro 20 milioni kama mshahara huku pia ikimhakikishia Messi kuwa angechukua asilimia 100 ya haki za mauzo ya sura yake. Hata hivyo kinda huyo aliyetua Barcelona akiwa na umri wa miaka 13, alikataa ofa hiyo na kuamua kuendelea kuwa mwaminifu kwa Barcelona.
Kwa upande wa Chelsea, inasemekana tajiri wa timu hiyo, Roman Abramovich, alikuwa tayari kulipa kiasi hicho cha pesa kwa ajili ya kumnyakua Messi na kumpeleka Stamford Bridge kuimarisha safu ya ushambuliaji ya timu yake.
Chelsea ambayo nayo inavaa Adidas, ilikuwa katika nafasi nzuri ya pili kumnasa Messi, lakini bado staa huyo wa Argentina aliamua kuitosa ofa hiyo na kuamua kubaki Catalunya ambako ameendelea kuwa mchezaji muhimu zaidi klabuni.
Kwa mujibu wa habari za uchunguzi, timu ya tatu ambayo inasemekana kuwepo katika dili hili ni Real Madrid ambayo nayo kwa muda mrefu sasa imekuwa ikitumia jezi za Adidas na ndio maana Gallardo akadokeza kwamba siku akiitaja timu ya tatu basi soka la Hispania litatingishika.
Hata hivyo, kabla ya Gallardo hajatoa maoni haya, tayari Rais wa Real Madrid, Fiorentino Perez, alishawahi kudokeza kwa utani kuhusu suala la timu yake kujaribu kuinasa saini ya Messi kama vile walivyowahi kufanya wakati walipomsajili staa wa zamani wa Barcelona, Luis Figo katika uhamisho ambao uliishtua dunia.
“Kama Barca haimpi mkataba Messi tuambieni tu. Tutamsajili,” alisikika akijigamba Perez.
Wakati huo huo, Figo mwenyewe alikaririwa akisema kwamba hakuna kisichowezekana kwa Messi kuichezea Real Madrid kama yeye alivyofanya katika siku za nyuma.
“Niliwahi kufikiria hivyo kwa sababu hili ni soko tu. Kama mtu anajiona hajaridhika, wakati klabu nyingine inapomtaka na iko tayari kulipa mkataba wake basi mambo yanawezekana. Hili ni soko huru,” aliongeza Figo.
Miongoni mwa wanamichezo maarufu wanaovaa Nike ni pamoja na LeBron James, Tiger Woods, Rafael Nadal, Serena Williams, Ronaldinho, Lance Armstrong, Michael Jordan, Cristiano Ronaldo na Maria Sharapova.
Miongoni mwa mastaa wenye mikataba binafsi na Adidas ni Messi mwenyewe, Andy Murray, Jo-Wilfried Tsonga, Mesut Ozil, Karim Benzema, Luis Suárez na Xavi Hernandez.