Adam : Muuaji wa Simba afunguka mazito
Muktasari:
Baada ya kutembea kwenye timu nyingi za FDL ikiwemo Majimaji FC hatimaye alijiunga na African Lyon na kufanikiwa kuipandisha Ligi Kuu mwaka 2017/18 ambapo walifanikiwa kumaliza msimu wa FDL wakiwa kileleni mwa msimamo.
MPACHIKA mabao wa JKT Tanzania, Adam Adam anasema raha ya mshambuliaji ni kufunga hasa kuzichapa Simba na Yanga, kwao huwa ni jambo kubwa na kuanza kufuatiliwa mara kwa mara katika michezo inayofuata.
Mifano ya wachezaji wa aina hiyo ipo na wa mwisho wa siku za karibuni alisajiliwa Ditram Nchimbi wa Yanga kabla ya msimu huu alikuwa akikipiga kwa mkopo Polisi Tanzania kutokea Azam FC, lakini alipoipiga Yanga mabao tatu akasajiliwa wakati wa dirisha dogo.
Adam naye baada ya kuichapa Simba kwenye kichapo cha bao 1-0 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam mwezi uliopita, anasema alifurahi sana japo ndoto yake bado haijatimia katika kutimiza malengo na sasa anaendelea kujifua ili siku moja aweze kucheza nje ya nchi.
“Sijawahi kuifunga Simba, hivyo nilichokuwa nakifanya ni kuwa karibu na lango la timu yao kwa kuangalia makosa ya ulinzi ambayo wanayafanya na sasa nimekuwa na mabao sita ndani ya msimu huu kwenye ligi,” anasema Adam
“Simba ni timu yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa, hivyo kocha alituelekeza namna ya kuwabana viungo wao ili wasipate nafasi ya kucheza mchezo waliouzoea.”
Anaongeza kuwa timu yoyote inayocheza na Simba lazima ijue itazidiwa kwenye kumiliki mpira, hivyo mpinzani anatumia muda mwingi kujilinda na kushambulia kwa kushtukiza. Mchezaji huyo alisajiliwa mwanzo wa msimu kutoka Tanzania Prisons, timu ambayo Abdallah Mohammed ‘Bares’ alikuwa akiifundisha msimu uliopita kabla ya kufungashiwa virago.
“Kocha ndio alihusika kunisajili akiwa Tanzania Prisons, japo aliondoka kabla sijacheza mchezo hata mmoja na baadaye akanichukua kuja hapa,” anasema.
Adam alianza soka tangu akiwa shule ya msingi huko Kilimanjaro na baada ya kumaliza alijiunga na Machava FC iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Tatu ngazi ya mkoa huo.
“Mwaka 2001 kulikuwa na mashindano ya Copa Coca-Cola yaliyofanyika Kilimanjaro ambayo Azam FC ilikuwa miongoni mwa timu shiriki na uongozi wa timu yetu ukawaomba ili nijiunge nao.”
Anasema: “Nilikubaliwa baada ya kufuzu majaribio na nikajiunga kwenye kikosi cha vijana kwa mwaka mmoja kisha nikatolewa kwa mkopo Lipuli FC ikiwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL).”
Anasema baadaye aliomba kuvunja mkataba na Azam ambao walikubali na akarudi tena Lipuli, kisha msimu uliofuata akatimkia Panone FC iliyokuwa ikinolewa na Fredy Felix ‘Minziro’, kisha akachukuliwa na JKT Tanzania mwaka 2015, lakini hakudumu kwani aliondoka na kwenda Mgambo Shooting.
Baada ya kutembea kwenye timu nyingi za FDL ikiwemo Majimaji FC hatimaye alijiunga na African Lyon na kufanikiwa kuipandisha Ligi Kuu mwaka 2017/18 ambapo walifanikiwa kumaliza msimu wa FDL wakiwa kileleni mwa msimamo.
“Nilihusika kuipandisha African Lyon Ligi Kuu nikiwa na mabao matano, kisha kutimkia Tanzania Prisons na kucheza nusu msimu huku nikifunga mabao 10, lakini niliumia mchezo wa mwisho dhidi ya Lipuli baada ya kuvunjika mkono, mchezo ambao sitaweza kuusahau maishani mwangu maana niliona unakatiza ndoto zangu.”
Tanzania Prisons nilisajiliwa na Kocha Mohamed Abdalah ‘Bares’ lakini sikufanikiwa kucheza akiwa hapo kwani aliondoka na sasa nimekutana naye hapa JKT Tanzania.”
Nyota huyo anasema kila mahali kuna changamoto na kwenye soka pia kuna vimbwanga ambavyo amekutana navyo na wenzake wakisimulia.
“Binafsi sijawahi kukutana na tukio ambalo linaashiria ushirikina ila katika moja ya timu nilizopita baadhi ya wachezaji walikuwa wakieleza na kulalamikia hilo.”