Abouba amekuja na mataji Bandari FC

Muktasari:

Baada ya mazoezi katika Uwanja wa mazoezi wa Mbaraki Sports Club, Abouba alisema ataichezea timu hiyo kwa moyo wake wote ili iweze kufanya vyema kwenye mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine ya vikombe.

GOLIKIPA mpya wa Bandari FC kutoka Rayon Sports ya Rwanda, Bashunga Abouba amesema ujio wake nchini kujiunga na timu yake hii mpya ni kwa ajili ya kuitumikia vyema akishirikiana na wenzake ili kuishindia mataji.
Baada ya mazoezi katika Uwanja wa mazoezi wa Mbaraki Sports Club, Abouba alisema ataichezea timu hiyo kwa moyo wake wote ili iweze kufanya vyema kwenye mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine ya vikombe.
“Niko nchini Kenya kuitumikia timu iliyonisajili na kuipatia sifa. Nina imani kubwa nitaweza kufanikiwa kutimiza lengo langu la kuwaridhisha waajiri wangu nikishirikiana na wachezaji wenzangu.”
Kuhusu hali yake ya mazoezi, Abouba alisema anajiona yuko tayari kuichezea timu yake hiyo kwani anaamini amefanya mazoezi wakati wa kutosha. “Nasubiri nafasi yangu nipate kuonyesha ujuzi wangu,” akasema.
Kocha Mkuu Ken Odhiambo alisema Abouba alifika Mombasa kwa usajili wakati wenzake tayari walikuwa wameanza mazoezi. “Ni kocha wake kusema yuko tayari, tuanze kumtumia kwa mechi zijazo.”
Bandari itacheza mchezo wao wa tatu wa Ligi Kuu dhidi ya Thika United Jumapili Uwanja wa Thika na Kocha Odhiambo anasema ana tamaa kubwa ya kurudi nyumbani na pointi zote tatu.