300 washiriki mbio za Tayac Arusha

Muktasari:
- Mbio hizo ambazo ni msimu wake wa pili zinashirikisha watoto kutoka shule mbalimbali za Mkoa wa Arusha walio na umri wa miaka sita hadi 14.
- Watoto hao wanachuana katika mbio fupi mita 100,200 na 400,mbio za kati mita 800,1500 na 3000,mbio za vihunzi mita 100,mbio za vijiti 4x100m, 4x400m pamoja na miruko na mitupo.
Arusha. Zaidi ya watoto 300 kutoka shule mbalimbali za Mkoa wa Arusha wameshiriki katika mashindano ya mbio za uwanjani ambazo zimeandaliwa na taasisi ya Tanzania Youth Athletics Championship (TAYAC) yakiwa na lengo la kuibua vipaji.
Mbio hizo zinafanyika kwa siku mbili leo Jumamosi na kesho Jumapili katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid yakishirikisha watoto walio na umri wa miaka sita hadi 14, ambao wanachuana kwenye mbio fupi mita 100,200 na 400,mbio za kati mita 800,1500 na 3000,mbio za vihunzi mita 100,mbio za vijiti 4x100m,4x400m pamoja na miruko na mitupo.
Akifungua mbio hizo mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini,Said Mtanda amesema kama serikali watashirikiana na wadau mbali mbali ambao wameonesha nia ya kuwekeza katika michezo kwani wana lengo nzuri ya kuandaa vijana ambao watakuja kuiletea heshima Taifa kwa miaka ya baadaye.

Amesema ni furaha kuona wadau wanajitokeza kukuza michezo hasa ile ambayo imesahaulika ambayo haipewi kipaumbele ikiwemo mbio za uwanjani hivyo ahatahakikisha kwa kipindi chote ambacho atakuwa jijini Arusha anashirikiana na wadau na viongozi mbalimbali hili kuendelea kunyanyua michezo katika jiji hilo.
“Tukitaka kukuza michezo tuanze na vijana wadogo serikali hapa wilayani na mimi nikiwa mkuu wa wilaya nitashirikiana na chama cha Riadha Arusha lakini pia nitashirikiana na taasisi mablimbali zenye lengo la kukuza vipaji”amesema Mtanda.

Mkurugenzi wa Tayac,Juliana Mwamsuva amesema mbio hizo kwa siku ya kwanza leo zimeshirikisha zaidi ya watoto 300 ambapo ushindani umekuwa mkubwa sana huku akiweka wazi kuwa utofauti wa mbio za mwaka huu na zile zilizopita ni kwamba michezo imekuwa mingi pia washiriki ni wengi.
Ameongeza kuwa matarajio yao ni kuona mashindano hayo yanakuza watoto wengi pia ushiriki kutoka mikoa mbalimbali itaongezeka tofauti na ilivyo sasa kwani matamanio yao ni kuona wanawatengeneza vijana wengi ambao watakuja kuleta medali na kuitangaza nchi kimataifa.
Kwa upande wa moja ya wazazi ambao watoto wao wameshiriki mbio hizo,Zainab Zahoro yeye anasema watoto wamekuwa wakikosa fursa ya kuonyesha vipaji kwani hakuna mtu wa kuwashika mikono lakini kupitia mbio hizo sasa anaamini wengi watakuwa wanajitokeza.