Yanga yavuta beki mwingine

MABOSI wa Yanga hawatanii, kwani wakati wakijiandaa kumleta straika wa kigeni, wamethibitisha kumchukua beki kisiki kutoka Mtibwa Sugar, jambo lililomshtua kocha wa timu hiyo, Vincent Barnabas aliyedai kama beki huyo anaenda Jangwani kwao itakuwa pigo.

Mchana wa leo Januari 11 Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Mashindano, Hersi Said ametuma picha kwenye mtandao wa Instagram ikimuonyesha beki huyo akiwa nae na mikataba mezani ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu.

Hata hivyo, Kocha Barnabas aliyewahi kukipiga Yanga, alisema kama ni kweli Job ataondoka kwenda Yanga basi kwao ni pengo na itachukuwa muda kuliziba ingawa watalazimika kutafuta mbadala wake.

Kauli ya Barnabas aliitoa jana Jumapili kisiwani hapa baada ya kuwepo taarifa za beki huyo kumwaga wino Yanga akisema kwamba anasubiri zaidi kupewa taarifa na uongozi wao kama kweli dili hilo limefanyika.

Barnabas anayekaimu nafasi hiyo wakati Kocha Mkuu Thiery Hitimana akiwa hajaanza kazi kwa kile kilichodaiwa kuwa kibali chake cha kazi bado kinashughulikiwa na mabosi wake, hivyo haruhusiwi kukaa benchi.

Akizungumza na Mwanaspoti, mjini hapa kabla ya kuanza safari ya kurudi Bara baada ya timu yao kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa kipigo cha 2-0 kutoka kwa Simba juzi usiku, Barnabas alisema Job ni beki mzuri ambaye amekuwa akiipambania timu nyakati zote hizo hivyo kama ataondoka timu itavurugika zaidi.

“Kiukweli ni kwamba mipango yetu haitaenda kama ilivyokusudiwa, sisemi kwamba waliopo sio wachezaji wazuri lakini kila mchezaji ana umuhimu wake kwenye timu, Job ni mpambanaji ametusaidia sana kipindi hiki ambacho timu yetu haiko vizuri kwenye mashindano,” alisema Barnabas aliyewahi kukipiga Kagera Sugar na Miembeni na kuongeza;

“Siwezi kuzuia kuondoka kwake na tutatafuta mbadala lakini ukweli pengo lake haliwezi kuzibika kwa haraka, kuondoka kwake kunaweza kutugharimu zaidi, mabosi wangu hawajanishirikisha lolote labda tukifika huko nitapewa taarifa kama kweli wamemuuza Job.

“Job ana mkataba, labda viongozi wamefanya biashara hivyo tusubiri kuona na kusikia nini kitatokea na ùkweli utakavyokuwa, maisha yataendelea ingawa tutatikisika kwa kiwango fulani,” alisongeza kocha huyo.

Kwa upande wa Job alithibitisha kuwepo kwa mchakato huo wa kutakiwa Yanga, japo alidai viongozi wa Yanga walikuwa wanafanya mazungumzo na mabosi wake kuona ni namna gani wataununua mkataba wake unaomalizika msimu ujao.

“Ni kweli kuna mazungumzo yanaenda baina ya viongozi kwasababu nina mkataba na Mtibwa, taarifa zimeenea kwamba nimesaini ila ukweli hadi muda huu (mchana wa jana Jumapili) sijasaini mkataba na Yanga na viongozi wangu hawajaniambia walipofikia,” alisema beki huyo aliyekuwapo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Vijana U17 kilichoshiriki Afcon 2017.

“Kama watakubaliana basi nitakuwa tayari kusaini Yanga na kuichezea timu hiyo, naipenda Mtibwa kwani imenilea kisoka na kufikia hapa nilipo sasa, hivyo nasikiliza uamuzi wao,” alisisitiza beki huyo.

Habari kutoka kwenye benchi la ufundi la Yanga, zilidai kuwa mpaka mchana jana walikuwa hawajanasa saini ya mchezaji huyo kwani mazungumzo ya kimkataba yalikuwa yanaendelea huku Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela naye akisema hawajamalizana na mchezaji huyo.

“Bado hatujamalizana maana kuna baadhi ya mambo tunaendelea kujadiliana,” alisema Mwakalebela.

Job ni mchezaji aliyepandishwa kutoka timu ya vijana ya Mtibwa Sugar na ameisaidia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kufanya vizuri.

Wakati dirisha dogo la usajili litafungwa Ijumaa, ndani ya Yanga kumekuwepo na taarifa mbalimbali za usajili kwa wachezaji wazawa lakini hadi sasa hakuna usajili rasmi uliotangazwa.