Yanga yapewa Warundi, Simba yala shushu..., Coastal, Azam FC ngoma nzito, JKU Mmh

Muktasari:
- Vigogo hivyo vimejua wapinzani watakaokutana nao katika msimu mpya wa michuano ya CAF kwa mwaka 2024-2025 baada ya droo kufanyika jana mchana jijini Cairo, Misri ambako wawakilishi wengine wa michuano hiyo, Azam, Coastal Union na JKU wakiwa na kibarua kizito kusaka nafasi ya kutinga makundi.
WAKATI Simba ikila shushu hadi raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikisubiri mshindi kati ya Uhamiaji ya Zanzibar na wawakilishi wa Libya, wababe wa soka nchini, Yanga wamepewa Vital’O ya Burundi katika mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Vigogo hivyo vimejua wapinzani watakaokutana nao katika msimu mpya wa michuano ya CAF kwa mwaka 2024-2025 baada ya droo kufanyika jana mchana jijini Cairo, Misri ambako wawakilishi wengine wa michuano hiyo, Azam, Coastal Union na JKU wakiwa na kibarua kizito kusaka nafasi ya kutinga makundi.
Simba na Yanga katika michuano ya msimu uliopita zote zikicheza Ligi ya Mabingwa ziliishia robo fainali, Mnyama akitolewa na waliokuwa watetezi walioenda kulibeba tena taji hilo, Al Ahly ya Misri, huku Wananchi waking’olewa kiutata na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Yanga ilitinga hatua hiyo chini ya kocha Miguel Gamondi aliyeipeleka kwanza makundi kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 25 ilipocheza mara ya kwanza michuano hiyo ilipobadilishwa kutoka Klabu Bingwa Afrika kuwa Ligi ya Mabingwa mwaka 1998, kisha ndipo ikavuka robo sambamba na watetezi Al Ahly.
Azam, JKU na Singida Fountain Gate zilitolewa mapema ziliposhiriki Kombe la Shirikisho kama ilivyokuwa kwa KMKM iliyoshiriki Ligi ya Mabingwa ikitokea visiwani Zanzibar.
Katika droo ya jana ambayo baadhi ya wadau wa klabu za Tanzania walitoa maoni na kueleza haitakuwa kazi nyepesi kwa timu tano zitakazoanza raundi za awali, kulinganisha na Simba itakayoanzia raundi ya pili.
Tuanze na Yanga, mabingwa hao wa Tanzania Bara wamepangwa kuanzia ugenini mjini Bujumbura, Burundi dhidi ya Vital’O na kama itapenya hatua hiyo baada ya kurudiana nao jijini Dar es Salaam itakuwa na nafasi ya kukutana na mshindi wa mechi kati ya SC Villa ya Uganda au Commercial Bank ya Ethiopia.
Azam iliyomaliza katika nafasi ya pili ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kushiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 10 ilipochezwa mwaka 2015 itaanzia nyumbani kuwakaribisha mabingwa mara 22 wa Rwanda, APR iliyopo nchini kwa sasa ikishiriki michuano ya Kombe la Kagame 2024.
Iwapo matajiri hao wa Chamazi, watafuzu katika mechi za raundi hiyo ya kwanza basi itakuwa na nafasi ya kukutana na mshindi wa mchezo kati ya JKU Zanzibar au Pyramids ya Misri, klabu anayoitumikia nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele ambayo msimu uliopita ilishiriki Ligi ya Mabingwa na kuishia makundi.
Kwa upande wa ratiba ya mechi za Kombe la Shirikisho, Coastal Union itaanzia kuchanga karata ugenini kwa kucheza dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola iliyopo Mashariki mwa Mji wa Luena, Angola kisha kumalizia mechi ya marudiano nyumbani.
Kama Coastal itavuka hapo, ikiwa inarudi kushiriki michuano ya CAF tangu mwaka 1989 iliposhiriki michuano ya Kombe la Washindi ambalo mwaka 2004 liliunganishwa na Kombe la CAF na kuzaliwa kwa michuano hiyo ya Shirikisho na itakuwa na kibarua kingine cha kukutana FC Lupopo ya DR Congo.
Wawakilishi wengine wa Zanzibar, Uhamiaji wana kibarua cha kuvaana na timu ya Libya ambayo bado haijafahamika kwa vile ligi ya nchi hiyo haijamalizika na kama itavuka salama katika raundi hiyo, itapata fursa ya kukutana na Simba katika mechi ya raundi ya pili kabla ya mshindi baina yao kwenda makundi.
Bingwa wa michuano hiyo ya Shirikisho kwa sasa ni Zamalek ya Misri iliyoifunga RS Berkane katika fainali zilizopigwa Mei mwaka huu na Uhamiaji imeshiriki michuano hiyo kuchukua nafasi ya Mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Zanzibar, Chipukizi ambayo ililiandikia Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF) isingekuwa na uwezo wa kushiriki michuano hiyo licha ya kupewa ushindi wa mezani dhidi ya JKU iliyofanya fujo kwenye mechi ya fainali iliyopigwa visiwani Pemba.
Mechi za awali za michuano hiyo, zitaanza kuchezwa kati ya Agosti 16-18 huku ile ya marudiano ikipigwa kati ya Agosti 23–25 ndipo michezo ya raundi ya pili itafuata baadaye Septemba na washindi kutinga makundi.
WASIKIE WADAU
Akizungumzia ratiba hiyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Hasheem Ibwe alisema, unaposhiriki michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa ni lazima kutegemea kukutana na timu imara, hivyo kupangiwa na APR ni moja ya maandalizi yao.
“Timu zote zilizokuwa hatua hii ni nzuri na ngumu kwa sababu ni mabingwa huko katika nchi zao walizotoka, kwa muonekano ni ratiba ngumu ila watu wanapaswa kutambua kwamba tumejiandaa kuleta ushindani ndio maana tumesajili wachezaji bora.”
Ibwe aliongeza, watahakikisha wanapambana kadri ya uwezo wao kwani moja ya malengo makubwa waliyojiwekea kama klabu ni kuhakikisha timu hiyo inafika hatua ya makundi kwa msimu ujao, hivyo hawana hofu na mpinzani yoyote aliye mbele yao.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Coastal, Omary Ayoub alisema, baada ya ratiba hiyo kutolewa watakaa chini na kufanyia tathimini ya kina juu ya mpinzani waliyepangwa naye japo kiujumla wamejipanga vizuri kuleta ushindani mkubwa msimu ujao.
Katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, jumla ya klabu 59 zitashiriki kutoka nchi 47 za Afrika huku kwa upande wa michuano ya Kombe la Shirikisho itakuwa na timu 52 ambazo kiujumla zinatoka katika nchi 41.
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisema wanaenda kukutana na mabingwa wa Burundi, Vital’O aliyoitaja kama timu nzuri ndio maana inashiriki Ligi ya Mabingwa na kwamba Yanga haina hofu na kuahidi kwenda kuendeleza ubora kwa kuwaheshimu.
“Michuano hii inashirikisha timu bingwa kama timu ni bingwa kwenye ligi yake basi hiyo ni bora tunaendelea na maandalizi nina imani na kikosi changu.”