Yanga, Simba ni vita ya ubora leo

Wednesday January 13 2021
ZENJI PIC 5
By Mwanahiba Richard

Unguja. Unaweza kusema ni ‘vita ya ubabe’ kwa watani wa jadi katika mchezo wa soka nchini, Simba na Yanga ambazo zinakutana katika mchezo wa pili msimu huu kwenye mashindano mawili tofauti.

ZENJI PIC 3

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa ni mechi ya mzunguko wa kwanza ambapo zilitoka sare katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Leo, timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa katika fainali ya Kombe la Mapinduzi ambalo ni mara ya 16 tangu lianzishwe 2007.

ZENJI PIC

Yanga ndiyo ya kwanza kutwaa ubingwa wa mashindano hayo mara tu yalipoanzishwa ilipoifunga Mtibwa Sugar katika fainali kwa mabao 2-1, huku Simba imetwaa mara tatu.

Advertisement

Awali timu hizo zenye mashabiki wengi nchini na nje ya Tanzania zilikutana mara ya kwanza katika fainali ya 2011 iliyokuwa ya msimu wa tano tangu kuasisiwa kwa michuano hiyo na Yanga ilikubali kichapo cha mabao 2-0.

ZENJI PIC 4

Msimu huu Simba na Yanga kila moja imepania kuonyesha kiwango bora ambapo Simba, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara watataka kuonyesha kwamba kutwaa ubingwa wa Bara mara tatu mfululizo na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hawakubahatisha.

Nayo Yanga inayoongoza Ligi Kuu pasipo kupoteza mechi itataka kudhihirisha kwamba inachokifanya Bara haibahatishi, hivyo ubingwa huo wanautaka.

ZENJI PIC 1

Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na timu hizo kuwa na mashabiki wengi, mwenyekiti wa kamati ya mashindano Khamis Said akisema hakutakuwepo masharti yoyote ya kuingiza mashabiki wachache uwanjani.

Akizungumzia mchezo huo, kocha mkuu wa Yanga, Cedric Kaze alisema kufika fainali ni jambo kubwa na lilikuwa ndilo lengo lao kuu.

“Tulikuwa tayari kucheza na timu yoyote ambayo ingeingia fainali, lakini tunafurahi zaidi pia kucheza na Simba, tutajiandaa kuona ni namna gani tunafanya vizuri kwenye mechi hiyo kuhakikisha tunatwaa ubingwa.

“Simba siyo timu mbaya na hata tulizocheza nazo hazikuwa vibaya ila katika mashindano ni lazima kujiandaa kwa kila mechi ili kupata matokeo mazuri, tunawaheshimu Simba,” alisema Kaze na kufafanua juu ya mshambuliaji Said Ntibanzonkiza.

“Anaendelea vizuri, lakini siwezi kusema mechi hiyo atacheza ama hatacheza kwani itategemea na namna atakavyoamka ingawa alianza kufanya mazoezi na wenzake.”

Kwa upande wake, kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema wametinga hatua hiyo wakiwa wamepambana na timu ngumu, hivyo wanaamini mechi hiyo watashinda.

“Tumepata matokeo mazuri katika mechi zetu zote zilizopita, hivyo hata hii ya fainali tunataka ushindi utakaotuwezesha kutwaa ubingwa wa Mapinduzi,” alisema Matola.

“Hakuna fainali rahisi sehemu yoyote ile, na kwa vile tunautaka huu ubingwa lazima tujiandae vizuri maana hata wapinzani wetu nao wanajiandaa, tunategemea kuwa ni mechi itakayokuwa na ushindani mkubwa na lazima bingwa apatikane.”

ZENJI PIC 2

Matola na Kaze kwenye mashindano hayo wameonekana kupenda kutumia mfumo wa 4-2-3-1 ili kupata matokeo mazuri.

Mbali na mfumo huo, Pia Kaze hupendelea kubadilisha mfumo kulingana na namna wapinzani wake walivyo ambapo hutumia 4-4-2 na 3-5-1-1. Mchezo huo unatarajiwa kuanza saa 2:15 usiku.

Advertisement