Yanga mwendo mdundo, Pacome, Mzize wawaka Sokoine

Muktasari:

  • Mchezo huo ulionekana kuwa wa presha kubwa kwa timu zote na kufanya mwamuzi wa mechi hiyo, Arajiga kutoa kadi mbili nyekundu kwa wachezaji wa pande zote, Kipa Metacha wa Yanga na Zabona wa Tanzania Prisons.

YANGA imesherehekea vyema 'bithidei' yake ya kutimiza miaka 89 kwa kishindo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons na kuendelea kujitanua kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiweka pengo la pointi 10 dhidi ya watani wao Simba.

Matokeo hayo yanawafanya mabingwa hao mtetezi kufikisha pointi 40 wakibaki nafasi ya kwanza huku Wekundu wa Msimbazi wakiwa na alama 30 licha ya Yanga kucheza mechi mbili zaidi.

Ushindi huo pia unaendeleza rekodi dhidi ya Wajelajela hao ambao hawajapata ushindi kwa mechi ya 13 sasa dhidi ya bingwa huyo mtetezi kwenye Ligi Kuu.

Kichapo hicho kwa Prisons kinakuwa cha kwanza kwenye Ligi Kuu na cha pili katika mashindano yake tangu akabidhiwe majukumu kocha Ahmad Ally aliyetokea KMC akichukua kiti cha Fred Felix 'Minziro' aliyetimkia Kagera Sugar.

Katika mchezo huo ambao umepigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa, Yanga ilionyesha kiwango bora huku mastaa Pacome Zouzoua na Macxi Nzengeli wakionekana kuelewana zaidi na kuwasumbua mabeki wa pembeni wa Prisons.

Yanga ilitangulia kupata bao dakika ya 14 kupitia kwa Clement Mzize akiunganisha vyema krosi ya Pacome na kuamsha mzuka kwa mashabiki wa timu hiyo waliofurika uwanjani hapo.

Dakika ya 18 mchezaji Joyce Lomalisa alijikuta kwenye kitabu cha mwamuzi Ahmed Arajiga (Manyara) kwa kuoneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu nahodha wa Prisons, Salum Kimenya.

Beki wa Prisons, Chilo Mkama naye alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 39 baada ya kumkwatua Nzengeli wakati akikokota na mpira eneo la katikati ya uwanja.

Prisons walijaribu kupeleka mashambulizi lakini mipira yao ilikosa wa kumalizia vyema, huku Yanga nao wakikosa mabao mawili ya wazi kupitia kwa Pacome aliyeshindwa kufunga baada ya pasi safi ya Nzengeli dakika ya 43, huku Nzengeli naye akikosa nafasi ya wazi dakika ya 45 akigongesha besela kwa shuti kubwa wakati langoni kukiwa hamna mtu.

Kabla ya kipyenga cha kwenda mapumziko, Yanga iliwanyanyua tena mashabiki kwa bao la pili lililofungwa na Pacome akipokea pasi safi ya Yao Kouassi baada ya shambulizi tamu lililoanzia golini na kumkuta mfungaji huyo na kwenda mapumziko Prisons wakiwa nyuma kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa presha kila timu kufanya mashambulizi na kusababisha kipa wa Yanga, Metacha kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea madhambi mchezaji wa Prisons akiwa amebaki pekee na kipa huyo katika dakika ya 59 na kumfanya kocha wa Yanga, Miguel Gamondi kumpumzisha Farid Mussa na kumuingiza kipa Aboutwalib Mshery.

Dakika ya 62, Prisons ilipata bao kupitia kwa Jeremia Juma aliyepiga mpira wa frii-kiki iliyoenda moja kwa moja wavuni lililomuacha Msheri asijue la kufanya. Frii-kiki hiyo ilitokana na kosa la Metacha lilimfanya alimwe kadi nyekundu.

Prisons ilimpumzisha Nurdin Chona ambaye nafasi yake ilizibwa na Ibrahim Abraham dakika ya 74, huku Yanga nao wakimchomoa Mzize na kumuingiza Guede huku beki wa Prisons, Nicodemas Mwaituka akionyeshwa njano dakika ya 83.

Gamondi aliwapumzisha pia Pacome na Nzengeli na nafasi zao kuchukuliwa na Gift Fred na Stephane Aziz Ki ambapo dakika ya 86 Zabona Khamis akionyeshwa nyekundu baada ya kadi mbili za njano kwa kujiangusha ndani ya boksi alipobanwa na beki Bakar Mwamnyeto.