Wazito FC kusubiri sana

Ni kubaya Wazito FC, wamesota

USALAMA wa Wazito FC kuendelea kukipiga Ligi Kuu Kenya msimu ujao unawahitaji kushinda mchezo wa mtoano ‘playoff’ ambayo hatima yake bado haijulikani.

Wazito FC ilimaliza nafasi ya 16 msimu uliopita hivyo kuepuka kushuka daraja moja kwa moja wakizipiku Mathare United na Vihiga Bullets.

Kwa kumaliza nafasi ya 16, Wazito FC itacheza mchezo wa nyumbani na ugenini katika playoff hiyo na timu itakayoshika nafasi ya tatu kwenye National Super League (NSL).

Wakati Ligi Kuu Kenya msimu 2021/22 ukiwa tayari umehitimishwa, NSL inayoshirikisha timu 20 bado inaendelea huku ratiba ikionyesha michezo ya mwisho imepangwa kuchezwa Julai 23 mwaka huu.

Hii inamaanisha Wazito FC inayonolewa na Fred Ambani itaendelea kusubiri sana kubaini ni timu gani ya NSL itakayoshika nafasi ya tatu kwa ajili ya mchezo huo wa playoff.

Kanuni za hivi sasa zinaruhusu uwepo wa playoff ila kwenye mabadiliko ya rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) iliyoandaliwa na Kamati ya Mpito na inasubiri kupitishwa na mkutano mkuu wa FKF imependekeza kuondolewa kwa playoff.

Aidha kitu kingine kitakachowafanya Wazito FC kusubiri muda mrefu kufahamu hatima yao ya kucheza Ligi Kuu Kenya msimu ujao ni giza nene lililotanda usimamizi wa soka nchini baada ya Kamati ya Mpito kumaliza muda wake wa wiki tano Juni 16 mwaka huu. Kamati ya Mpito iliyokua na wajumbe 12 ikisaidiwa kutekeleza majukumu yake na secretariate ya wajumbe sita ilikua inasimamia Ligi Kuu Kenya na NSL.

Macho sasa yameelekezwa kwa Waziri wa Michezo, Balozi Amina Mohamed, kutoa mwelekeo huku Kenya ikiendelea kutumikia kifungo cha muda usiojulikana kilichotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kufuatia Serikali kuivunja FKF na kumtimua ofisini rais wake Nick Mwendwa.