Waarabu wamfuata Nabi Dar

Waarabu wamfuata Nabi Dar

YANGA bado haijawapa mikataba mipya makocha wao, lakini kama kuna kitu kitawashtua basi ni ujio wa ofa moja kubwa kwa kocha mkuu Nasreddine Nabi ambaye kama hawatajiongeza dakika yoyote atayeyuka kutokana na fedha ndefu iliyowekwa na waarabu kutoka Morocco.

 Taarifa za uhakika kutoka Morocco ni kwamba klabu ya AS FAR Rabat inasaka saini ya kocha huyo raia wa Tunisia kwa nguvu kubwa akarithi mikoba ya kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroeck.

FAR Rabat imemaliza ya tatu katika ligi ya msimu uliopita, kitu ambacho hakijawafurahisha mabosi wa klabu hiyo na kuamua kuachana na Sven, aliyeiwavusha Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2020-2021 na kuwapa mataji mawili misimu miwili iliyopita ambapo kwa sasa ametua Abha Club ya Saudi Arabia.

Rabat ambaye ni timu ya jeshi imemwekea mezani Nabi mshahara mkubwa unakadiriwa kufikia Dola 40,000 (Sh 93 milioni) kwa mwezi ambao unaweza kuwa ni mara nne ya ule anaolipwa na Yanga.

Juzi Rais wa klabu hiyo, Mohamed Haramou akitangaza mpango wa maboresho ya timu yao kwa msimu ujao alisema kuna makocha wawili wanafanya nao mazungumzo akiwemo kocha Mtunisia mwenye uraia pacha na Ubelgiji, kocha mwingine akiwa raia wa Ufaransa.

“Tutakuwa na maboresho makubwa ya kikosi chetu kuekekea msimu ujao,Rabat sio timu ya kusindikiza timu zingine, tutaleta wachezaji bora watakaorudisha nguvu ya timu hii, pia tunafanya mchakato wa kuleta kocha mkubwa ambaye atakuwa sahihi kwa klabu hii, tunaweza kumpata mtu kutoka Tunisia mwenye uraia wa Ubelgiji au Mfaransa,” alisema Haramou akizungumza na vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Mmoja wa maafisa wa FAR Rabat ameshatua nchini kimyakimya kuja kuzungumza na Nabi ambaye aliiwezesha Yanga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu bila kupoteza sambamba na kutwaa Kombe la ASFC na Ngao ya Jamii.

Yanga bado haijawapa mikataba Nabi na wasaidizi wake Cedric Kaze, Milton Nienov wa makipa na wengine katika benchi hilo ukiwa ni mtihani mkubwa wa Rais mpya wa Yanga Injinia Hersi Said.

Hatua ngumu kwa Yanga ni endapo Nabi ataondoka ambapo itawalazimu kukuna vichwa katika kumpata kocha ambaye atachukua nafasi yake huku muda ukiwa umebaki mdogo kabla ya kuanza mashindano.