Vanga United FC yatamba Kisiwa Koja Kaboom Cup, fainali lazima

Saturday January 16 2021

WACHEZAJI wa timu ya Vanga United FC waliingia kiwanja cha Kiwegu kucheza mechi ya ugenini dhidi ya Kiwegu Stars FC wakielekeza juhudi zao zote kuhakikisha wanashinda pambano lao hilo ili wapate kufuzu kwa fainali ya mashindano ya Kisiwa Koja Kaboom Cup.

Katika mechi hiyo ya nusu fainali ya iliyochezwa Jamamosi iliyopita ya Januari 9, 2021, Vanga iliyotoka mji wa Vanga, kilomita chache kutoka uwanja huo wa Kiwegu, ilionekana mwiba tangu filimbi ya kwanza wanasoka wake wakipania kuipeleka timu yao fainalini.

Kocha wa timu hiyo , Abdalla Juma aliliambia Mwanaspoti walipoondoka Vanga walikuwa na shughuli moja pekee ya kuitimiza nayo ni kuhakikisha wamepata tikiti ya kucheza fainali ya mashindano hayo.

“Niliamini kutokana na moyo ulioonyeshwa na wachezaji wangu tangu wakijitayarisha kwa mchezo huo dhidi ya Kiwegu Stars FC, nilijua kwa uwezo wa Mungu, tutaibuka washindi na kupata fursa ya kucheza fainali itakayopepetwa hapo Januari 31,” akasema Juma.

Kwa mashabiki wa Kiwegu Stars FC waliofika hapo uwanjani, walikubali mapema kuwa timu yao haitaweza kuwashinda wageni wao ambao walianza mechi kwa kasi na kulivamia lango la wapinzani wao mara kwa mara hadi wakaibuka washindi kwa mabao 3-1.

Mkufunzi Juma alisema wamekuwa wakijitayarisha kwa mashindano hayo mapema na walipofika nusu fainali, alikuwa hana wasiwasi wowote kwani alikuwa amewasoma vizuri wapinzani wao.

Advertisement

“Sitaki kutoboa siri ya jinsi niliweza kuwafanya wapinzani wetu wasiwe kukabiliana na mchezo wetu, lakini njia niliyotumia sipendi kuieleza kwani tuna mpinzani wa mwisho wa kucheza nao katika fainali ambayo tuna hamu tuibuke washindi,” akasema Juma.

Nahodha wa timu hiyo, Juma Boi amesema wanajiandaa vilivyo kwa mazoezi kabambe ili waweze kucheza vizuri Zaidi ya walivyofanya dhidi ya Kiwegu ili kuhakikisha wanaibwaga Jego Cranes FC katika fainali ili kombe hilo lifika Vanga.

“Tuna imani kubwa kama juhudi zetu zitazaa matunda. Tulianza kujitayarisha mapema kwa mashindano hay ana tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika fainali. Nia yetu ni kuhakikisha tunabeba taji hili na kulileta kwetu,” akasema Boi.

Nahodha huyo anasema kuwa kikosi chao kina wachezaji wengi wenye tajriba ya kusakata soka la hali ya juu wakipatiwa nafasi ya kufanya hivyoi. Kikosi cha timu hiyo kina Chamira Said, Kingoma Salim na Shosi Uzeri.

Wanasoka wengine ni Hamad Mwasoza, Nasir Ali, Bahaa Jamuhuri, Chacha Hamisi, Said Mulele, Majjam Abdallah, Juma Boi, Hatibu Mohamed, Babuu Majjam, De Gea Suleiman, Boka Issa, Ferrar Juma, Said Mubai, Hassan Mohamed na Marwa Jamuhuri.

Nahodha Boi anasema kuwa kwao hawana cha kudharau, timu yoyote wanayopangiwa hujitayarisha na kutaka kushinda. “!Tunachohitaji sisi ni kuhakikisha tunapata ushindi kila mechi tunayoicheza,” akasema.

Mtayarishi wa mashindano hayo ya Kisiwa Koja Kaboom Cup Kanda ya Vanga-Kiwegu, Juma Gomb era almaarufu Bilawewe anasema anatarajia kutakuwa na patashika siku ya fainali kwani timu zote mbili za Jego Cranes na Vanga United ni nzuri na zinacheza soka La hali ya juu.

“Ninaamini Jumapili ya Januari 31 wakati wa mechi ya fainali, timu hizo zitaweza kuonyesha ubora wao na timu itakayocheza vizuri zaidi ndiyo itakayibuka washindi,” akasema Bilawewe aliyeahidi kuwa kutakuwa nna wageni wengi mashuhuri watakaoshuhudia fainali hiyo.


Imeandikwa na ABDULRAHMAN SHERIFF, VANGA

Advertisement